DODOMA. Waziri wa Afya Ummy Mwalimu, amekutana na kufanya mazungumzo na KIDO, ambaye ni Balozi wa Kampeni ya Holela-Holela itakukosti.
Kampeni ya Holela-Holela itakukosti inasisitiza mbinu kamilifu ya ‘Afya Moja’ kushughulikia tatizo la UVIDA na magonjwa ya zuonotiki na ilizinduliwa jijini Dar es Salaam mwishoni mwa mwezi uliopita kwa uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana Wizara ya Afya, Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na Wizara ya Mazingira huku ikifadhaliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) kupitia mradi wa Breakthrough ACTION.
Akizungumza jijini Dodoma baada ya kufanya mazungumzo na Balozi KIDO, Waziri wa Afya Ummy amesisitiza juu ya usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (UVIDA) na magonjwa ya kipaumbele ya zuonotiki (magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu), ambayo kampeni ya Holela-Holela Itakukosti imelenga.
“Naomba nichukue fursa hii nitoe wito kwa jamii kuwa Mtanzania anaweza kufanya mambo machache tu kukabiliana na UVIDA, kama vile kupata na kufuata ushauri wa mtaalamu wa afya kabla ya kutumia dawa, kutumia dozi ya dawa kikamilifu kama unavyoshauriwa na mtaalam wa afya, kufuata maelekezo ya mtaalam wa mifugo/kilimo juu ya matumizi sahihi ya dawa kwa mifugo/mimea, na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na usafi wa mazingiria kwa ujumla,” amesema na kuongeza:
“Suala la UVIDA ni tatizo kubwa sana, na athari zake ni kama vile ugonjwa kujirudia rudia na kuchukua muda mrefu kupona, kuenea na kusambaa kwa vimelea sugu vya magonjwa dhidi ya dawa, ulemavu na hata kifo.
“Mbali na hapo kuna athari za kiuchumi kama vile kutumia gharama kubwa kwenye matibabu, hivyo kupungua kwa pato binafsi, la familia na taifa,” amesema.
Amesema Serikali inafanya jitihada kabambe za kukabiliana na UVIDA, ikiwemo kuzindua kampeni ya Holela Holela itakukosti, inayolenga kuongeza uelewa juu ya UVIDA na kuleta mabadiliko chanya ya tabia ili kukabiliana na UVIDA katika jamii.
Kwa Upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa USAID nchini Tanzania Alex Klaits, amesisitiza umuhimu wa juhudi za pamoja, akisema: “Kampeni inaonesha jukumu muhimu la ushirikiano katika kuleta athari chanya na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu, ikiwaleta pamoja wadau wa afya moja kutoka sekta mbalimbali kupambana na UVIDA na magonjwa ya zuonotiki,” amesema.