Waziri wa Nishati Zambia atembelea gesi asilia

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Nishati nchini Zambia Mhandisi Himba Cheelo amefanya ziara ya kikazi kutembelea mitambo ya kupokelea GESI ASILIA Kinyerezi inayomilikiwa na TPDC .

Mhandisi Cheelo amesema kuwa lengo la ziara yake ni kujifunza namna Tanzania imepiga hatua kubwa katika suala la uzalishaji na usambazaji wa gesi asilia  kwa matumizi mbalimbali kama vile uzalishaji wa umeme, viwandani, kwenye Magari na manyumbani.

Cheelo, amesema  Zambia imefanya mabadiliko makubwa katika suala zima la uagizaji na uingizaji wa mafuta ya Petroli ambapo kufikia Septemba 30, 2023 serikali ya Zambia ilijiondoa rasmi katika jukumu la kuagiza mafuta ya petroli na kuachia jukumu Hilo kwa sekta binafsi.

“Ziara yetu inalenga kujifunza namna ambavyo Tanzania imepiga hatua katika suala zima la gesi asilia  pamoja na uagizaji wa mafuta ya Petroli” amesema Cheelo.

Mhandisi Cheelo alipokelewa na Mwenyeji wake ambae ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati Heri Mahimbali.

Aidha, Mhandisi Cheelo alipata fursa ya kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme Kwa kutumia gesi asilia ya Kinyerezi inayomilikiwa na shirika la umeme nchini Tanesco.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati (Tanzania) Heri Mahimbali amesema “tunafurahi kupokea ugeni huu na tupo tayari kuwapatia ushirikiano kwa ajili ya wao kujifunza namna ambavyo Serikali yetu inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia imepiga hatua katika eneo la nishati hasa gesi asilia, umeme pamoja na mafuta ya Petroli”.

Aidha,  Cheelo ambae yupo nchini Kwa ziara ya kikazi ya siku tatu, atatembelea pia kituo cha kujaza gesi asilia kwenye Magari kilichopo Ubungo jijijni Dar es Salaam,Karakana ya DIT inayohusika na kubadili Mifumo ya magari, Taasisi ya uagizaji wa Mafuta (PBPA), Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Nishati na Maji-EWURA pamoja na kampuni Tanzu ya kuzalisha nguzo za umeme za Zege inayomilikiwa na TANESCO

Habari Zifananazo

Back to top button