Wenyeviti Tandahimba watakiwa kuzingatia misingi ya uongozi

WENYEVITI wa Vijiji na Vitongoji wilayani Tandahimba mkoani Mtwara wametakiwa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia misingi bora ya uongozi ili kuleta ufanisi wa kazi yao.

Akizungumza wilayani Tandahimba wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wenyeviti hao, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba Sosthenes Luhende amesema kupitia mafunzo hayo wenyeviti hao wazingatie misingi ya uongozi ili wakatekeleze vema majukumu yao ya kila siku katika kuwatumikia wananchi kwenye maeneo yao.

‘’Swala la msingi sisi kama viongozi kupitia mafunzo haya ikawe chachu katika kutekeleza majukumu yenu kwa ufanisi kwa kuwatumikia vema wananchi kwenye maeneo yetu tukizingatia misingi bora ya uongozi, kufanya hivi itasaidia kuwatendea haki wananchi wetu’’amesema Luhende

Advertisement

Mada mbalimbali zimewasilishwa wakati wa mafunzo hayo ikiwemo uendeshaji wa vikao na mikutano katika ngazi ya vijiji, mitaa, na vitongoji.

Hata hivyo uibuaji, upangaji na usimamizi wa miradi shirikishi ya jamii, usimamizi na udhibiti wa fedha katika mamlaka ya serikali za mitaa, uongozi na utawala bora.

Akizungumza kwa niaba ya wenyeviti hao wa vijiji na vitongoji, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanhyanga ‘C’ wilayani humo Karim Mtimbuka amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao hayo ya kila siku.

‘’Naipongeza sana serikali kwa hatua hii mzuri iliyochukua kuona umuhimu wa kutupatia sisi viongozi mafunzo haya ambayo yanaenda kuleta tija wakati tunapotekeleza majukumu yetu haya ya uongozi’’amesema Mtimbuka