“Wezi wa mil 200/- za bodaboda wasakwe”

MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mrisho Mashaka Gambo amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kusaidia kufanikisha upatikanaji wa Sh milioni 200 zilizotapeliwa na waliokuwa Viongozi wa Umoja wa Waendesha Bodaboda Jiji la Arusha miaka minne iliyopita.

Gambo amesema hayo wakati wa Mkutano Mkuu wa Waendesha Bodaboda Jiji la Arusha unaofanyika leo Ijumaa Disemba 27, 2024,mbele ya mgeni rasmi ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM Taifa, Mohammed Kawaida.

Gambo ametoa fedha taslimu Sh milioni 10 kwa ajili ya kuwasaidia madereva bodaboda hao kuweza kusajili na kuendesha chama chao cha ushirika kilichozinduliwa leo jijini Arusha na Mohammed Kawaida.

Advertisement

Katika maelezo yake, Gambo amesema umoja huo katika uongozi uliopita walikabidhiwa pia pikipiki 200 ambapo kila Kata ilipata Pikipiki nane za mikopo na ushahidi wa mikopo hiyo na marejesho ya fedha zipo kwenye Benki ya NMB ambayo ndiyo iliyokuwa inatumika kwa kutolea na kufanya marejesho ya mikopo hiyo kwa wanakikundi wa Jumuiya ya Bodaboda.

Gambo licha ya kukiri kuwa wahusika wa wizi huo wanajulikana na bado wapo hai, ameahidi kutoa Sh milioni 1 kwa mwananchi atakayetoa taarifa zitakazofanikisha kukamatwa kwa wahusika walioiba fedha hizo zaidi ya milioni 200 za madereva bodaboda.

Wakati wa hotuba yake, Mwenyekiti wa UVCCM Taifa Ndugu Kawaida, ameliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Taasisi ya kupambana na kudhibiti Rushwa TAKUKURU pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama Mkoa wa Arusha kuhakikisha wahusika wote wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.