Wiki ya AZAKI kufanyika Arusha Juni

DAR-ES-SALAAM : WIKI ya Asasi za Kiraia (AZAKI) kwa mwaka 2025 imepangwa kufanyika mkoani Arusha kuanzia Juni 2 hadi 6.Tukio hili linaendelea kuwa jukwaa muhimu linalowakutanisha wadau mbalimbali kujadili dira ya maendeleo ya Taifa huku likihimiza ushiriki mpana wa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa The Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, ametumia uzinduzi wa wiki hiyo jijini Dar es Salaam kuwataka wananchi kupaza sauti zao kwa kutoa maoni kuhusu mwelekeo wa Taifa, hasa wakati huu ambapo Tanzania ipo katika mchakato wa kuandaa dira ya maendeleo ya mwaka 2050.

Rutenge amesema kuwa zaidi ya washiriki 500 wanatarajiwa kushiriki katika mijadala na warsha mbalimbali zitakazojikita katika mustakabali wa nchi, na kusisitiza kuwa nafasi hii ni adhimu kwani dira ya Taifa hutungwa mara moja tu kwa miongo miwili au zaidi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa CBM International na Mwenyekiti wa Kamati za Azaki, Nesia Mahenge, amesema wiki hiyo inalenga kutathmini changamoto na mafanikio ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka Tanzania bara na Zanzibar, pamoja na kuweka mikakati ya kuzitatua.

Mahenge amesema Azaki zitatumia fursa hiyo kupanga mikakati ya kutafuta rasilimali na ushirikiano kwa ajili ya maendeleo ya jamii huku wakitoa mfano wa mataifa mengine yanayojifunza kutoka kwa mafanikio ya Tanzania.

SOMA: Dira ya Maendeleo 2050 kuwekeza rasilimaliwatu

Amesema kuwa masuala ya kisiasa ya kimataifa, kama kusitishwa kwa misaada na Marekani, hayatapunguza azma yao ya kutatua changamoto za ndani.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Association NGOs, Adamsoni Nsimba, amesema kuwa wiki hiyo itasaidia kuwajengea uwezo wananchi, kuwalinda walaji na kusukuma mbele sera na sheria zinazolenga haki za kijamii kwa maendeleo jumuishi ya taifa.
Mwisho

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button