Wilaya ya Tanganyika wafungua njia chuo cha VETA

Wilaya ya Tanganyika wafungua njia chuo cha VETA

HALMASHAURI ya Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi, imetoa ekari 20 kwa ajili ya ujenzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Wilayani Tanganyika.

Akizungumza wakati walipotembelea eneo hilo, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika, Shaban Juma amesema wamejipanga kuhakikisha chuo hicho kinajengwa.

Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amesema watahakikisha wanasimamia ujenzi kwa kuwa kuna vijana wengi waliohitimu darasa la saba na kidato cha nne, hivyo kukamilika kwa chuo hicho itakuwa mkombozi kwa vijana wengi wilayani humo.

Advertisement

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa VETA Kanda ya Kusini Magharibi, Shomari Omary,  amesema wameamua kujenga chuo hicho Tanganyika baada ya kugundua kuna uhitaji mkubwa.

Omary amesema wameridhishwa na mandhari ya eneo hilo na mikakati ya ujenzi itaanza mwishoni mwa mwezi huu endapo watapata hatimiliki ya eneo hilo.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Tanganyika, Hamad Mapengo ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.