Wilaya zote Mtwara kufikiwa na mitungi ya gesi

MTWARA: MKOA wa Mtwara unatarajia kupokea mitungi ya gesi 1675 ambayo itasambazwa katika wilaya zote za mkoa huo na kuuzwa nusu bei kwa wananchi ili kuwawezesha kutumia nishati safi na salama.

Mitungi hiyo imetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan kama ruzuku kwa bei ya mitungi kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).

Mkurungezi wa umeme vijiji kutoka REA Mhandisi Jones Olotu amesema hayo leo Octoba 28 wakati wa uzinduzi wa umeme katika kijiji cha Makome Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara.

Advertisement

“Mitungi hiyo inauzwa Kwa nusu bei kwa ajili ya kuwawezesha wananchi kutumia nishati safi na salama kwa afya zao lakini pia kutunza mazingira,” amesema na kuongeza kuwa fedha za mitungi hiyo imetolewa na Raisi Samia Suluhu Hassan.

Mwezi Mei mwaka huu Rais Samia alizindua mkakati taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kuhakikisha kuwa asilimia 80 ya watanzania wanatumika nishati hiyo.

Hatua hiyo inakuja miezi michache baada ya kiongozi huyo kuongoza mkakati kwa nchi za Afrika kuwawezesha wanawake barani humu kuanza kutumia nishati safi ya kupikia, wakati aliposhiriki Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (COP 28) huko Dubai.

Ndani ya mkakati huo ambao ni wa miaka 10, Rais Samia anataka kuwepo nguvu ya pamoja kuanzia wahisani wa kimaendeleo, taasisi za umma na sekta binafsi ili kuongeza chachu kufikia malengo yake.