Wizara tano kuchambua hoja za walimu wasio na ajira

SERIKALI imesema itaunda timu ya wataalamu itakayojumuisha wizara tano kuchambua waraka wa unaojiita Umoja wa Walimu Wasio na Ajira (NETO).

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa mma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema hayo katika Mji wa serikali Mtumba, Dodoma.

Kikao hicho kilishirikisha Ofisi ya Rais, Utumishi, Ofisi ya Rais, Tawala za Miko na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Wizara ya Elimu Sayansi na Teknolojia na viongozi wa NETO.

“Ninamuelekeza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, Juma Mkomi kuunda timu ya wataalamu kutoka Ofisi ya Rais Utumishi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ofisi ya Rais-Mipango na Uwekezaji, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Wizara ya Fedha ili kuchambua makala hiyo ili tuweze kutumia mapendekezo yao kupata suluhu ya upungufu wa ajira kwa walimu,” alisema Simbachawene.

Aidha, alisema serikali ina haki ya kumsikiliza kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na kwa kuzingatia misingi ya 4R ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Simbachawene alisema Serikali ya Awamu ya Sita inazingatia misingi ya Falsafa ya 4R (Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga upya) hivyo ujio wa viongozi wa NETO na utayari wa viongozi wa serikali kuwasikiliza viongozi hao ni jitihada zinazosadifu uzingatiaji wa falsafa hiyo.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alisema utaratibu wa usaili unaleta ushindani, haki na kuondoa mwanya wa upendeleo kwa wasailiwa.

“Mapendekezo yenu ni mazuri na sisi kama serikali tunasubiri timu iliyotajwa na Simbachawene ifanye kazi ya kupitia na kuchambua makala hiyo na kisha kuleta ushauri wa namna bora ya kuboresha mchakato wa ajira za walimu,” alisema Profesa Mkenda.

Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Utumishi, Juma Mkomi alisema ofisi yake iko tayari kuunda timu hiyo na itatoa taarifa ndani ya kipindi cha siku 30 hadi 45 zilizoelekezwa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button