Wizara yaja na mpango uendelezaji eneo la Sinza

WIZARA ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakuja na mpango wa uendelezaji upya eneo la Sinza jijini Dar es Salaam (Sinza Redevelopment Plan 2024 – 2044.).

Taarifa hiyo imetolewa leo na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii wakati wa uwasilishaji taarifa ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha Ardhi (KKK).

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo mbele ya kamati hiyo, Mratibu wa Mradi wa KKK, Godfrey Machabe amesema wizara inaandaa mpango wa uendelezaji upya wa maeneo kongwe katika Mkoa wa Dar es Salaam

Advertisement

“Wizara kwa kushirikiana na Halmashauri ya Manispaa Ubungo pamoja na wadau wengine imeandaa Mpango wa Uendelezaji Upya eneo la Sinza (Sinza Redevelopment Plan 2024 – 2044.),”amesema Machabe

Amebainisha kuwa mpango wa uendelezaji upya katika eneo hilo  ni mkakati wa kina kwa ajili ya kufufua maeneo ambayo yamezorota na kupoteza thamani na uhalisia.

Kwa mujibu wa Mratibu huyo, mpango huo unatekelezwa eneo la Sinza kutokana na sababu mbalimbali kama vile ukuaji wa kasi na majengo marefu, ongezeko kubwa la watu na shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii.

Mpango huo umepanga kujumuisha mabadiliko ya matumizi ya ardhi, kujenga na kuboresha miundombinu pamoja na kuboresha huduma za jamii na miundombinu ya huduma  za jamii kama vile Usafiri, maji safi, maji taka, maji ya mvua, umeme, taka ngumu, mifumo ya gesi, nishati ya umeme na mawasiliano.

Kwa upande wake, Kamati ya kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii chini ya mwenyekiti wake Timotheo Mzava imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha ardhi unaotekelezwa na Wizara ya Ardhi kwenye maeneo mbalimbali nchini.

“Tumeridhishwa na utekelezaji mradi wa KKK ukiwemo huu mpango wa kuendeleza maeneo kongwe ikiwemo eneo la Sinza,” amesema Mzava.

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geophrey Pinda amesema wizara yake inafuatilia maeneo ya miji mikongwe kwa lengo la  kuona namna ya kuyaboresha ili kuendana na kasi ya ukuaji wa maendeleo.

Akigeukia mradi wa KKK katika Mwaka 2023/24, Naibu Waziri wa Ardhi amesema wizara yake ilihuisha akaunti ya Mfuko wa Maendeleo ya Ardhi (PDRF) kwa ajili ya utekelezaji miradi ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi, mfuko alioueleza kuwa utakuwa ukitoa fedha kwa halmashauri kutekeleza miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi.

Kwa mujibu wa Pinda, mfuko huo umeandaliwa mwongozo wa uratibu na utekelezaji kwa ajili ya kufanya kazi kwa ufanisi zaidi.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi Maliasili na Utalii imepokea na kujadili taarifa za wizara ya Ardhi zinazohusu Utekelezaji Mradi wa Kupanga, Kupima na Kumilikisha Ardhi (KKK), Hatua iliyofikiwa katika Uandaaji wa Sera ya Ardhi pamoja na taarifa ya hatua iliyofikiwa kwenye Uanzishwaji wa Mamlaka ya Sekta ya Milki nchini (Real Estate Authority).