TIMU ya Yanga itacheza mchezo wa kwanza wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC, Agosti 9, 2023 kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga huku Simba ikikwaruzana na Singida Fountain Gate siku inayofuata kwenye uwanja huo huo.
Yanga iliifunga Azam FC bao 1-0 katika mchezo wa fainali ya Kombe la FA na sasa zinakutana tena kwenye uwanja huo huo wa Mkwakwani Tanga.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana na Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), mchezo wa Ngao ya Jamii unashirikisha timu nne na fainali zake zitachezwa Agosti 13 kwenye uwanja huohuo.
Ngao ya Jamii ambayo huashiria kuanza kwa msimu mpya wa ligi 2023/2024, hivyo mashabiki wa Tanga watashuhudia sasa timu zote kubwa zikichezwa kwao ikiwa ni siku chache tangu kushuhudia fainali ya FA.
Singida Fountain Gate inakutana na Simba ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mara moja na sare moja katika michezo ya Ligi Kuu msimu uliopita.
Kwa upande wa Azam FC wao watakuwa na kumbukumbu mbaya ya kufungwa kwenye fainali ya FA iliyochezwa Tanga mwezi uliopita na kwenye michezo ya Ligi Kuu walifungwa na Yanga mchezo mmoja na sare moja msimu uliopita.
Ngao ya Jamii mashabiki watazishuhudia timu hizo zikiwa na mastaa wengine wapya waliosajiliwa msimu huu na wengine waliohama kutoka timu moja kwenda nyingine.
Ukiacha wachezaji wapya, Yanga watakuwa na kocha mpya, Miguel Gamondi na Azam FC itakuwa chini ya kocha mpya kutoka Senegal, Youssouph Dabo.
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza rasmi Agosti 15, mwaka huu na Agosti 16 mechi za awali za michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika zitaanza kuchezwa.
Comments are closed.