DAR ES SALAAM: KLABU ya Yanga kwa kushirikiana na GSM Foundation wametoa Sh milioni 200 na tani 100 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa kituo kipya cha kuhudumia wazee chini ya Taasisi ya Petra Elderly Center.
Akielezea utekelezaji huo, Mkuu wa GSM Foundation, Faith Gugu amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana na Yanga wameamua kuiunga mkono ikiwa ni utimizaji wa ahadi waliyoitoa kwa taasisi hiyo iliyoasisiwa na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Stergomena Lawrence Tax.
“Kimsingi tunatimiza ahadi tuliyoahidi Oktoba 26, 2024 tulipoalikwa Ukumbi wa Super Dom, Masaki kwenye chakula cha jioni kwaajili ya kuchangia taasisi ya Petra Elderly Center ambapo tuliguswa na wazo hilo,” amesema.
Kwa upande wake, Rais wa Young Africans SC, Mhandisi Hersi Said amesema, dhamira kubwa ni kuunga mkono jitihada za sekta binafsi, hususani katika kuigusa jamii ya kundi la wazee.
“Tunaamini kituo hiki kitaenda kugusa kundi hili kubwa na nipenda kuisihi jamii kuitika katika masuala kama haya yanayoigusa jamii,” amesema Mha. Hersi.
Kwa upande wake, Meneja wa Petra Elderly Center, Mussa Juma ameishukuru Yanga na GSM, hata hivyo amesema kituo hicho ni kwaajili ya kutathmini na kulinda utu wa wazee pia vijana watapata nafasi ya kujifunza busara kutoka kwa wazee.
“Kituo hiki kitaanza kuhudumia wazee 50 huku wanufaika wakitarajiwa kuwa watu 1,300 kwa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani,” amesema meneja huyo.
Ameongeza kuwa siku za usoni, programu hiyo inatarajiwa kufanyika katika maeneo mbalimbali kama Mwanza, Arusha na Zanzibar.