DAR ES SALAAM; YANGA leo watakuwa wanaikaribisha Fountain Gate FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa KMC, Mwenge Dar es Salaam.
Katika mchezo huo Yanga wanakuwa na ari ya kuendeleza ushindi mnono baada ya kuifunga Dodoma Jiji kwa mabao 4-0 katika mchezo uliopita na Fountain Gate walifungwa na Namungo FC kwa mabao 2-1.
Yanga inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu wakiwa na pointi 36 baada ya kucheza michezo 14 wakati Fountain Gate wanashika nafasi ya sita, wakiwa na pointi 20 baada ya kucheza michezo 15.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha Mkuu wa Yanga, Sead Ramovic alisema wanakwenda kwa tahadhari kwani wamepata muda wa kuwafuatila wapinzani wao na wamebaini wana uwezo wa kutumia nafasi.
“Tunajua namna ambavyo wamekuwa wakicheza, lakini sisi tumejidhatiti kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, tutahakikisha tunakuwa makini kuanzia dakika ya kwanza ili tufanikiwe kupata pointi tatu,” alisema Ramovic.
Naye Kocha Mkuu wa Fountain Gate, Mohammed Muya alisema wamerekebisha makosa yaliyosababisha wafungwe katika mchezo uliopita na sasa asingependa kuona inajirudia tena.
“Baada ya mchezo uliopita tumepata muda wa kurejesha utimamu kwa wachezaji wetu, hatutegemei kesho ‘leo’ kurudia makosa, tutatumia nafasi hii kuonesha tumekua kiasi gani tunapocheza na timu yenye ubora kama hii,”
Aliongeza kuwa anakwenda kumkabili mshindani ambaye ameshamtafiti uimara na udhaifu wake, hivyo anategemea matokeo mazuri.
Mchezo mwingine ni kati ya Coastal Union na KMC katika Uwanja wa Shekhe Amri Abeid, Arusha.