Yanga ubingwa, Pamba kisasi

YANGA watakuwa wageni wa Pamba Jiji kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza leo.
Wakati Pamba Jiji wakiwa wenyeji wa Yanga, Tabora United wataikaribisha Dodoma Jiji, Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora.
Wakati Yanga wakiibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Mashujaa, Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma, Pamba walipata sare ya mabao 2-2 na Singida Black Stars, Uwanja wa Liti mkoani Singida.
Tabora wenyewe wakiwa ugenini walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Tanzania Prisons, Uwanja wa Sokoine, Mbeya huku Dodoma Jiji wakipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fountain Gate.
Macho na masikio ya mashabiki wengi wa soka nchini yatakuwa Uwanja wa CCM Kirumba kwenye mchezo kati ya Pamba na Yanga.
Katika mchezo wa awali Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam Yanga ilipata ushindi wa mabao 4-0, hivyo itakuwa nafasi nzuri kwa Pamba kulipa kisasi kwenye uwanja wake wa nyumbani.
Wakati Pamba wakiwa na malengo ya kulipa kisasi na kujiweka kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, ushindi kwa Yanga utakuwa na maana ya kuwa kwenye mazingira mazuri ya kutetea ubingwa wao kwa mara ya nne mfululizo.
“Kesho (leo) tutacheza na Pamba, naelewa wanahitaji pia pointi tatu na wanauwezo wa kushambulia na kufunga lakini sisi tuna mbinu kwa ajili ya mchezo huo ambayo tumeifanyia mazoezi lakini hapa sitaweka wazi mbinu hiyo ni siri yangu kwa ajili ya kesho (leo),” alisema Kocha Mkuu wa Yanga, Miloud Hamdi akiuzungumzia mchezo huo wa leo.
Kwa upande wake, Kocha Mkuu wa Pamba, Fred Felix ‘Minziro’ alisema wapo katika mpango wa kutoka nafasi za chini hadi juu kwenye msimamo wa ligi, hivyo wamejipanga vizuri kupata matokeo.
“Kama nilivyosema bado tupo nafasi za chini tunapigana kupanda juu, na sisi kwenye dirisha dogo tumefanya usajili wa kila nafasi kuwa na wachezaji wawili ninaamini itakuwa mechi ya aina yake,” alisema Minziro, nahodha wa zamani wa Yanga.
Yanga inaongoza ligi ikiwa na pointi 55 baada ya kucheza michezo 21 huku Pamba wakiwa na pointi 22 wakishika nafasi ya 12 katika michezo 21 waliyocheza



