Yanga yawataka Kagera Sugar muda wowote

KIKOSI cha timu ya Yanga kimeanza kupiga hesabu kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Kagera Sugar Februari 1, kikizitaka alama zote tatu.

Mchezo huo unatarajiwa kufanyika kwenye Uwanja wa KMC  Complex, Dar es Salaam huku Yanga ikihitaji ushindi  ili kutengeneza mazingira ya kutetea ubingwa wa Ligi Kuu iliyouchukua kwa misimu mitatu mfululizo.

Meneja wa Yanga, Walter Harrison amesema anaamini kikosi chao kitapata matokeo mazuri kwenye mchezo huo.

“Maandalizi yanaendelea vizuri ukizingatia kuwa msimu huu tunataka kuendelea tulipoishia kusaka mataji yote ya ndani, mechi zipo nyingi ambapo kila mchezaji atapata nafasi ya kusaidia timu kufikia malengo.

“Jambo la kushukuru ni kwamba wachezaji wapo katika hali nzuri isipokuwa Yao Kouassi ambaye anaendelea kuuguza majeraha, kikubwa mashabiki wetu wajiandae kuja Uwanja wa KMC Complex ili kupata burudani ya kutosha,” amesema.

Menja huyo wa Yanga amesema hawauchukulii mchezo wowote kwa masihara na badala yake watahakikisha wanapata matokeo mazuri kwani malengo ya klabu kwa sasa ni kushinda michezo yote ya mzunguko huu wa pili.

“Huu mzunguko wa pili hatutakiwi kupoteza, tunatakiwa kuwa makini kutafuta matokeo ambayo yatatufanya kurejea kwenye nafasi yetu ya kuongoza ligi. Tunajua kazi haitakuwa rahisi ndio maana tunaendelea kufanya maandalizi ya nguvu,” amesema.

Walter amesema kutokana na hali ya wachezaji kuwa imara suala la mabadiliko ya kikosi yatakuwa chini ya Kocha Mkuu Sead Ramovic kulingana na aina ya wapinzani wanaokwenda kukutana nao.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button