WATU 1,648,219 kati ya 8,599,228 waliochoma chanjo ya Pfizer na Sinopharm katika kipindi cha mwezi Julai hadi Agosti 14 hawajarudi kupata chanjo ya pili, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Wizara ya Afya.
Taarifa ya Wizara ya Afya inafafanua kuwa katika kipindi cha mwezi Julai watu 1,712,107 walichoma chanjo ya Pfizer na kati yao watu 449,416 sawa na asilimia 26 hawakurudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Pfizer kama inavyotakiwa.
Pia kati ya watu 2,439,250 waliopata chanjo ya Sinopharm watu 325,982 sawa na asilimia 13 hawajarejea kupata dozi ya mwisho.
Katika kipindi cha Agosti Mosi hadi 14, watu 416,869 kati watu 1,719,296 walichoma chanjo ya Pfizer sawa na asilimia 24 ya waliotakiwa kurudi hawajarudi.
Hali kadhalika, katika kipindi hicho watu 455,952 kati ya watu 2,728,575 waliopata chanjo ya Sinopham ambayo ni sawa na asilimia 17 pia hawajarudi kwa ajili ya dozi ya pili ya Sinopharm.
Juliana Mshama, Mratibu – Elimu kwa Umma na Ushirikishaji Jamii wakati wa dharura (RCCE) kutoka Wizara ya Afya amesema, Wizara ipo kwenye ufuatiliaji kuhakikisha wote wanapata chanjo kamili.
Amesema lengo la serikali ni kuchanja watanzania 59,744 wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea kwa siku.
Idadi ya watu waliopata chanjo kamili tangu ilipozinduliwa na Rais Samia Suluhu Julai 28, 2021 ni 15,960,643 sawa na asilimia 51.92. ya wananchi zaidi ya milioni 30.74 wenye umri wa miaka 18 na kuendelea waliokusudiwa.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Afya, wanaume walipata chanjo tangu zilipoanza kutolewa Tanzania bara ni asilimia 54 huku wanawake wakiwa wastani wa asilimia 46.
Aidha, ametaja mikoa iliyo chini ya asilimia 50 ya watu wake kupata chanjo ni Pwani, Iringa, Katavi, Singida, Rukwa na Songwe huku Dar es Salaam, Arusha, Dodoma na Mwanza ikiwa kinara kwa wakazi wake kupata chanjo kwa asilimia 85.
“Mkakati wa serikali kwa ni kutoa chanjo kwa angalau asilimia 70 ya Watanzania wenye umri wa miaka 18 na kuendelea ifikapo Desemba, 2022,” amesema.
Idadi ya dozi zilizopokelewa ni 24,376,529, na dozi 24,376,529 sawa na asilimia 99 tayari zimesambazwa na dozi zilizotumika hadi August 14, 2022 ni 21,370,545.