RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Umoja wa Ulaya (EU) ni mshirika muhimu katika juhudi za kukuza uchumi hivyo wataendelea kushirikiana.
Dk Mwinyi alitoa tamko hilo katika Wilaya ya Mjini Unguja wakati akifungua kongamano la biashara la Zanzibar na Ulaya.
Alisema serikali inajitahidi kuandaa mazingira mazuri ya uwekezaji nchini ili wawekezaji wanaokuja wawekeze katika mazingira bora na endelevu.
Dk Mwinyi alisema miongoni mwa hatua inazochukua ni pamoja na uimarishaji na ujenzi wa viwanja vya ndege, bandari na miundonbinu ya barabara ili wawekezaji wawekeze kwa matumaini na mafanikio.
Aidha, serikali inaendelea kuchukua hatua kuondoa vikwazo katika uwekezaji kuvutia wawekezaji ikiwa ni pamoja na kuondoa urasimu na kuwa na miongozo na sera bora za uwekezaji nchini.
Dk Mwinyi alisema EU ina mchango mkubwa kwa maendeleo ya sekta ya uwekezaji na ustawi wa maisha ya wananchi.
Alisema uwekezaji wa Ulaya visiwani Zanzibar unachangia asilimia 31 ya miradi yote ya uwekezaji iliosajiliwa unaofikia thamani ya Euro bilioni 2.8 na kutoa fursa za ajira 19,000.
Dk Mwinyi alizitaja sekta sita ambazo serikali imezipa kipaumbele katika uwekezaji ni uchumi wa buluu, uvuvi wa bahari kuu, utalii, mafuta na gesi, kilimo, teknolojia ya habari na mkawasiliano na miundombinu ya barabara.
Alihimiza washiriki wa kongamano hilo walitumie kuibua maeneo mapya ya ushirikiano baina ya serikali na sekta binafsi na EU na kubaini njia bora za kutatua changamoto ziliopo hivi sasa kwenye uwekezaji.
Dk Mwinyi alishuhudia kasainiwa mkataba wa ushirikiano baina ya EU na Mamlaka ya Uwekezaji ya Zanzibar (ZIPA) sanjari na kuzindua Ripoti ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya hapa Zanzibar ya Mwaka 2023