SMZ yajivunia ushirikiano na India

ZANZIBAR : Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema miongoni mwa mafanikio makubwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayojivunia ni ushirikiano wa Kidiplomasia uliopo baina yake na Serikali ya India kwa kuanzishwa tawi la Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras, Zanzibar.

Mwenyekiti huyo wa Baraza la Mapinduzi, ameyasema hayo alipozungumza na Balozi wa India nchini, Mhe. Bishwadip Dey aliyefika kujitambulisha Ikulu Zanzibar.

Amesema, Chuo Kikuu cha Teknolojia cha IIT Madras ni fursa muhimu kwa sekta ya elimu Zanzibar itakayoleta mageuzi makubwa ya mifumo na kukuza teknolojia nchini.

Advertisement

Rais Dk. Mwinyi ameiomba India kupitia mtandao mkubwa wa teknolojia walionao na kwa uweledi wa mitandao ya kijamii kuendelea kuitangaza Zanzibar Kimataifa kupitia tawi la Chuo hicho duniani pamoja na sekta za biashara na uwekezaji.

Naye, Balozi  Bishwadip Dey alimuhakikishia Rais Dk. Mwinyi kuendeleza historia ya ushirikiano uliopo wa pande mbili hizo hasa kwenye kuboresha sekta za Biashara, Uchumi, Utalii na Uwekezaji pia alimuahidi Rais Dk. Mwinyi kuendelea kupokea wafanyabiashara wakubwa kutoka India, wenye nia ya kuwekeza Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

SOMA: Ziara ya Rais Samia India yafungua fursa nchini