Zanzibar mbioni kuzalisha umeme wake wenyewe

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akizungumza na uongozi wa Kampuni ya ‘WAPCOS Limited’ ya India, uliofika Ikulu Zanzibar

ZANZIBAR: SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema inahitaji uwekezaji mkubwa wa sekta za Maji na Umeme ili kuongeza ufanisi wa huduma za uhakika kwenye sekta hizo.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu iliyotolewa leo imetanabahisha kuwa Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo alipozungumza na uongozi wa Kampuni ya ‘WAPCOS Limited’ ya India, uliofika Ikulu Zanzibar.

Advertisement

Dk Mwinyi amesema hadi sasa Zanzibar inapokea megawati 110 za nishati ya umeme, kutoka Tanzania Bara, hivyo amesema, Serikali inadhamira ya kuzalisha umeme wake wenyewe na iko tayari kushirikiana na kampuni yoyote itakayokuwa tayari ili kuanza hatua za upembuzi yakinifu.

Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi akiwa pamoja na RK Agrawal Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya ushauri WAPCOS, Ikulu Zanzibar

Pia, Dk Mwinyi amesema, Zanzibar inahitaji utafiti wa kina wa uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa nishati hizo kwa kuangalia zaidi uwekezaji na huduma za uhakika.

Soma pia: https://habarileo.co.tz/gesi-asilia-kuwafikia-watanzania-wote/

Dk. Mwinyi ameikaribisha kampuni ya “WAPCOS Limited” endapo inavutiwa kufanya kazi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Amesema, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na ya India ni wadau wakubwa kwenye huduma za jamii na zimekua zikishirikiana kwenye nyanja mbalimbali za Maendeleo ikiwemo elimu.

Naye, Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya “WAPCOS Limited, Rajni Kant Agrawal amesema kampuni yao imejikita zaidi kutoa huduma za ushauri hasa kwenye nishati za umeme, maji na miundombinu na kueleza kuwa wako tayari kushirikiana na Serikali kwenye uwekezaji wa sekta hizo.

Amesema, kwa Tanzania tayari kampuni hiyo inafanya kazi maeneo ya Dar es Salaam na mengine ikiwemo Zanzibar.