Zanzibar yapiga ‘bao’ kiwanda cha mwani Afrika

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla amebainisha kuwa serikali imekamilisha ujenzi wa kiwanda kikubwa cha kuchakata mwani ambacho ni cha kwanza kwa nchi za Afrika.

Abdulla alisema hayo wakati wa kuelezea mafanikio ya mpango wa Uchumi wa Buluu katika utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa kipindi cha miaka minne kuanzia Novemba, 2020 hadi Desemba, 2024.

Alisema pia serikali kupitia Kampuni ya Mwani Zanzibar imekamilisha ujenzi wa kiwanda cha kusarifu mwani katika eneo la Chamanangwe Pemba ambacho kimegharimu Sh bilioni 8.5 chenye uwezo wa kuchakata tani 30,000 za mwani mkavu kwa mwaka na kuongezea thamani ya zao la mwani.

Advertisement

Abdulla alisema kiwanda hicho kimeweza kutoa ajira rasmi zipatazo 25,000 na zisizo rasmi takribani 66,000. Alisema pia serikali imeanza ujenzi wa kiwanda cha kutengenezea chakula cha samaki kilichopo Unguja ili kushajihisha ufugaji wa samaki na kuwaondolea usumbufu wa huduma hiyo.

Abdulla alisema serikali imetoa boti 1,077 kwa wakulima wa mwani na wavuvi zaidi ya 5,000 Unguja na Pemba ambazo ndani yake zina vifaa mbalimbali zikiwemo, vifaa vya kutafutia samaki, GPS, mishipi nyavu pamoja na makoti ya kujiokolea.

Alisema juhudi hizo zimesababisha uzalishaji wa mwani kuongezeka kutoka tani 12,594 za Sh bilioni 10 hadi kufikia tani 19,716 za Sh bilioni 16.4 sawa na ongezeko la asilimia 94 na uzalishaji wa samaki ambao umeongezeka kutoka tani 38,107 za Sh bilioni 205 kwa mwaka 2020 hadi kufikia tani 80,085 za Sh bilioni 569.07.

Abdulla alisema serikali imekamilisha ujenzi wa jiko na Soko la Samaki Malindi la Dola za Marekani milioni 14 huku ukarabati wa Soko la Samaki Nungwi, Unguja na Tumbe, Pemba umekamilika na masoko hayo yanahudumia wananchi.

Akizungumzia uwekezaji wananchi kiuchumi, Abdulla alisema serikali imeboresha mazingira bora kwa wafanyabiashara wa Unguja na Pemba kwa kujenga miradi mikubwa ya masoko na stendi ikiwemo ujenzi masoko ya Mwanakwerekwe, Jumbi, Chuini kwa Nyanya na ujenzi wa vituo zaidi ya 14 kwa wajasiriamali. Alisema mitaji ya wafanyabiashara na wajasiriamali imeongezeka na kuwawezesha kufanyabiashara kwa kuwapa mikopo isiyo na riba. Abdulla alisema serikali imetenga zaidi ya Sh bilioni 34 kwa ajili ya kuwapatia mikopo hiyo na hadi sasa mfuko huo umeshatoa Sh bilioni 31 kwa Unguja na Pemba.