Zanzibar yaweka mkazo katika ulinzi na malezi bora

ZANZIBAR: SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imetangaza kuwa haitenganishi watoto na familia zao, lakini inachukua hatua za kuwalea watoto wanaokumbwa na changamoto kama vile kutupwa au kutelekezwa.
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Anna Athanas Paul, alitoa kauli hiyo katika kikao kilichofanyika Makao ya Watoto Kurasini, Dar es Salaam.
Waziri Paul alisema kuwa, wakati Serikali imejenga nyumba ya kulea watoto katika eneo la Mazizini, hakuna watoto wa mitaani Zanzibar isipokuwa kuna familia zinazoishi katika mazingira magumu.
Alisisitiza kwamba Serikali inachukua hatua za kukomesha unyanyasaji wa watoto ambao hushiriki katika biashara ndogo ndogo, na inawapa huduma za msingi kama elimu na afya.
Naibu Waziri huyo alitoa wito kwa jamii kuacha tabia ya kuwatumikisha watoto katika kazi za nyumbani, akisema kuwa watoto wote chini ya umri wa miaka 18 wanahitaji malezi bora na haki zao za msingi.
Aidha, aliweka bayana kuwa watu wanaotaka kuwachukua watoto hufanyiwa taratibu kupitia Wizara hiyo ili kuhakikisha watoto hao wanapata malezi bora. SOMA: Gwajima avipa vituo vya kulelea watoto utaratibu

Katibu Mkuu wa Wizara, Abeida Rashid, alifafanua kwamba Zanzibar inawalea watoto 26 katika nyumba ya Mazizini, na inawapatia huduma zote muhimu, pamoja na ruzuku za matumizi ya kila mwezi.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ustawi wa Jamii, Sabiha Filfil Thani, alihimiza umuhimu wa usalama na ulinzi wa watoto, na kupongeza wahudumu kwa kazi zao nzuri.
Meneja wa Makao ya Watoto Kurasini, Twaha Kibalula, alielezea historia ya makao hayo, akisema yalianzishwa mwaka 1966 na yanatoa huduma kwa watoto walio katika mazingira hatarishi.
Aliongeza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu, kituo kimehudumia watoto 209, na sasa kina watoto 82, huku kikifanya miradi ya uzalishaji mali kama kilimo na ufugaji ili kusaidia mahitaji ya watoto.



