SERIKALI imewaagiza wamiliki na waendeshaji wa vituo vya kulea watoto nchini kote kuhakikisha kila mtoto anayepokelewa anaandaliwa mpango wa huduma wa kumuandaa kuondoka makaoni.
Pia imepanga kuanzisha mjadala wa wadau ili kuja na sheria ya malezi ambayo itawalazimisha wazazi kutimiza wajibu wao kwa malezi ya watoto. Maelekezo hayo yametolewa jijini hapa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima (pichani)wakati wa maadhimisho ya miaka 20 ya makao ya watoto yatima wasiojiweza walioko Kijiji cha Matumaini jijini Dodoma.
Alisema serikali inasisitiza umuhimu wa mtoto aliyepo makaoni kuandaliwa kisaikolojia kupitia huduma zinazotolewa na mipango ya kumuondoa makaoni. Alisema mchakato huo usipofanyika ipasavyo hufanya watoto kuona makao ni nyumbani kwao na sehemu ya kudumu.
“Watoto wanajikuta wanalelewa hadi utu uzima na mara nyingi wakitoka makaoni hushindwa kujitegemea na kuishi katika familia zao. “Niwaagize wamiliki na waendeshaji wa makao kote nchini kuhakikisha kila mtoto anayepokelewa anaandaliwa mpango wa huduma unaojumuisha mpango wa kutoka makaoni na taarifa zote zihifadhiwe katika jalada la mtoto,” alisema.
Dk Gwajima pia amewaagiza maofisa ustawi wa jamii wote nchini kuhakikisha agizo hilo linatekelezwa katika maeneo yao na msajili wa makao, kamishna wa ustawi wa jamii kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi wafanye ufuatiliaji ipasavyo.
Aidha, Dk Gwajima alisema wizara ina mpango wa kuandaa mjadala mpana ikiwa ni mwelekeo wa kuja na sheria ya makuzi na malezi ambapo pamoja na mambo mengine itamlazimisha mzazi kutimiza wajibu wake. Alisema wazazi na walezi wanatakiwa kutimiza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa sheria, tamaduni na mila za Kiafrika za kuhakikisha watoto wanatimiziwa mahitaji yao ya msingi na kulindwa.
Alisema idadi ya watoto 145 wanaolelewa katika makao hayo ni sehemu ya watoto 24,454 wanaolelewa katika makazi 324 yaliyosajiliwa nchini yakiwemo makao mawili ya Serikali ya Kurasini Dar es Salaam na Kikombo Dodoma.
Aidha, Dk Gwajima alimwelekeza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kushirikiana na mamlaka zinazohusika kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya utozwaji kodi katika miradi iliyobuniwa ambayo inaathiri utumiaji wa mapato katika kukidhi mahitaji ya watoto wanaolelewa makaoni hapo au kutoa ushauri stahiki.
Pia aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa madarasa na maabara katika Shule ya Sekondari Maria De Mattias inayomilikiwa na makao hayo na kutoa mchango wa Wizara wa Sh milioni tano kuunga mkono ujenzi huo. Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dodoma, Beatus Kinyaiya aliiomba serikali kuona namna ya kuondoa kodi kwenye misaada ambayo inakuja kwa ajili ya kusaidia maendeleo ya Kijiji cha Matumaini.
Akisoma risala ya makao hayo, Msimamizi wa Utawala wa Kijiji cha Matumaini, Balthazar Sungi alisema makao hayo yaliyoanzishwa mwaka 2002 yanatumia mfumo wa familia kwa wanakaya kujitolea kuwatunza kama watoto wao.
Alisema tangu kuanzishwa kwa makao hayo, watoto 350 wamehudumiwa na kwa sasa makao yana watoto 145 wanaoishi katika familia 13 ambapo watoto 63 ni wa kiume na 83 ni wa kike.