‘Zingatieni usawa wa kijinsi kuleta maendeleo’

Jamii imetakiwa kuzingatia usawa wa kijinsia pamoja na haki za binadamu hususani kwa wanawake kushiriki katika nyanja mbalimbali, ili kuleta maendeleo nchini.

Wito huo umetolewa na Julieth Sandy ambaye ni mtaalamu wa masuala ya kijinsia katoka taasisi ya ESP, wakati wakifungua mafunzo ya usawa wa kijinsia na haki za binadamu kwa baadhi ya viongozi mbalimbali wa Kata ya Nsimbo.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mradi wa uwezeshaji kupitia ujuzi, unaotekelezwa katika chuo cha maendeleo ya wananchi Msaginya, wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake hasa vijana wa kike, ambao wamepitia changamoto mbalimbali zikiwemo mimba za mapema, umasikini ambao umewanyima fursa ya kuendelea na masomo katika mfumo rasmi au kupata uwezo wa kujiajiri ama kuajiriwa.

Amesema mradi huo unalenga kuwawezesha vijana wa kike waliopo katika mazingira magumu angalau 720 nchini, ambapo vijana 60 katika kila chuo cha kati kwenye vyuo 12 vilivyochaguliwa, watawezeshwa kupata ujuzi katika vyuo hivyo vya maendeleo ya wananchi.

Amesema baada ya kumaliza masomo wametengeneza mfumo wa kuweza kumsaidia binti aliyehitimu kwa kupewa kitendea kazi ama mtaji au vyote kwa pamoja.

Naye alkado William, mtoa elimu wa kwa jamii kutokea asasi ya Tuelimike, amesema mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miaka 7 kuanzia 2021 hadi 2028, ili kuweza kuifikia sehemu kubwa ya jamii na kuleta chachu ya mabadiliko katika jamii juu ya mitazamo hasi, kuhusu wanawake na kuwawezesha kufikia ndoto zao.

Amesema wakati wanapeleka mradi huo kwa wananchi walipata changamoto ya mitazamo hasi kwa baadhi ya kaya, ambapo jamii iliamini mradi huo umekuja kumuinua mtoto wa kike na kumdidimiza mtoto wa kiume, lakini baada ya utekelezaji wa mradi uelewa umeongezeka na wanaamini hadi mradi huo kukamilika walau asilimia 70 hadi 80 ya wanawake watafaidika.

 

Habari Zifananazo

Back to top button