Zuberi Maulid ashinda kwa kishindo Spika Baraza la Wawakilishi

BARAZA la Wawakilishi Zanzibar leo limemchagua Zuberi Ali Maulid wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwa Spika wa Baraza hilo, baada ya kupata kura 53 sawa na asilimia 94 ya kura zote zilizopigwa.
Uchaguzi huo umefanyika katika kikao cha kwanza cha baraza hilo Chukwani Mjini Unguja,kinachoashiria mwanzo wa shughuli rasmi za Baraza la Wawakilishi la Awamu ya Kumi na Mbili. SOMA: Wajumbe Baraza la Wawakilishi wazuru TCRA kujifunza
Wagombea wengine waliokuwa wakichuana katika kinyang’anyiro hicho ni Naima Salum Hamad wa chama cha UDP na Suleiman Ali Khamis wa ADC ambao hawakupata kura, huku Chausiku Khatib Muhammed wa NLD akipata kura tatu. Baada ya ushindi huo, Spika mpya Zuberi Ali Maulid ameapishwa na kuanza rasmi majukumu yake ya kuliongoza baraza hilo.
Baada ya uchaguzi wa Spika kukamilika, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanatarajiwa kuendelea na hatua ya kumchagua Naibu Spika leo hii, kabla ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kuhutubia na kulizindua rasmi baraza hilo kesho, kwa mujibu wa Katiba ya Zanzibar.



