Zungu aunga mkono nishati safi

DODOMA: SPIKA wa Bunge, Mussa Azzan Zungu, ameuagiza Umoja wa Wabunge Wanawake (TWG) kutumia ushawishi wao mitaani kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kulinda afya za wananchi na mazingira.
Akifungua mafunzo ya umoja huo yaliyoandaliwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) jijini Dodoma, Spika Zungu amewataka wabunge hao kuvunja dhana potofu zilizopo kwenye jamii.
“Kuna dhana zisizo za kweli kwamba nishati safi ni ghali, ni ngumu kutumia, na inaharibu ladha ya chakula. Nendeni mkaondoe dhana hizi ili tufikie azma ya serikali ya kuwa na asilimia 80 ya watanzania wanaotumia Nshati safi ifikapo mwaka 2034,” amesema Spika Zungu.

Naye, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, amesema STAMICO imekuwa msaada mkubwa kupitia nishati yake mbadala ya Rafiki Briquettes ambayo ni rafiki kwa mazingira na ina gharama nafuu.
Dk. Kiruswa alibainisha kuwa mkaa huo unawasaidia wananchi kupunguza gharama na kuepuka magonjwa hatari ya macho na mapafu yanayosababishwa na moshi wa kuni au mkaa wa miti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Migodi na Huduma za Kihandisi wa STAMICO, Mhandisi Baraka Manyama ambaye alimuwakilisha Mkuu Mtendaji DkVenance Mwasse, amesema Shirika hilo lina mkakati wa kuongeza viwanda zaidi nchini ili kupanua uzalishaji wa mkaa huo wa kisasa, lengo likiwa ni kukidhi soko la ndani na kuanza kuuza nchi za nje.
STAMICO inaendelea na juhudi za kuhamasisha na kuhakikisha matumizi ya Nishati Safi yanaenea kwa kasi katika kona zote za Tanzania.



