Zuwena Senkondo: Afurahia sera ya Barrick kunufaisha Watanzania kupitia sekta ya madini

“SERA ya ushirikishaji Watanzania katika mnyororo wa uchumi wa madini sambamba na miradi ya kusaidia jamii, ni moja ya masuala yanayonivutia katika kazi yangu kwa kuwa nafurahi kuona sekta ya madini inayovyoendelea kunufaisha wananchi,” anasema Zuwena Senkondo.
Senkondo ni Ofisa Mwandamizi wa Barrick Bulyanhulu anayeshughulika na mahusiano ya kijamii, utatuzi wa migogoro na kusimamia miradi ya kijamii inayotekelezwa na kampuni hiyo kupitia fedha za uwajibikaji kwa jamii.
Anasema anaipenda kazi yake kwa kuwa inamwezesha kushughulika na wananchi na anafurahia kushuhudia mabadiliko yao kutokana na uwekezaji kwao kupitia miradi ya uwajibikaji kwa jamii (CSR) kwenye maeneo yao.
Moja ya miradi iliyotekelezwa na Barrick Bulyanhulu ambayo itaacha alama kwa miaka mingi hata ikiwa mgodi utafungwa, anaitaja kuwa zaidi iko katika uimarishaji wa sekta za afya, elimu na upatikanaji wa maji safi na salama.
“Kinachofurahisha zaidi miradi hii yote imelenga kukomboa wanawake kwa kuwa ndio waathirika wakubwa wa huduma za afya zikilegalega, kuachwa nyuma kielimu pia ndio wahanga wakuu wa changamoto ya ukosefu wa maji katika maeneo yao,” anasema Senkondo katika mahojiano hivi karibuni.
Baadhi ya miradi ya jamii inayotekelezwa na Barrick Bulyanhulu ambayo ameshiriki katika utekelezaji wake anaitaja kuwa ni uboreshaji wa miundombinu ya elimu inayolenga kumuongezea msichana ufanisi katika kusoma na kujifunza kama ujenzi wa hosteli, maabara na madarasa katika shule za sekondari Bugarama, Mwingiro, Msalala, Nyang’hwale na Bulyanhulu.
Miradi mingine ni kusaidia vikundi vya wanawake kurasimisha biashara zao ili kufanya kazi na mgodi na wakandarasi wake (ufugaji, kilimo); kuwezesha vikundi vya wanawake kutafuta masoko ya bidhaa wanazotengeneza; kusaidia programu za kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa kike na uanzishwaji wa jukwaa la wafanyabiashara linalowezesha kupatiwa elimu ya ujasiriamali.
Kwa upande wa afya, Barrick imetekeleza mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya cha Bugarama ambacho kina wodi kubwa ya kujifungua wanawake. Kituo hicho kimekuwa kikihudumia zaidi ya wananchi 20,000 wanaoishi eneo hilo na vitongoji jirani.
Pia Senkondo anabainisha kuwa Barrick imekuwa ikifanya kazi na taasisi mbalimbali za serikali kukabiliana na changamoto ya upatikanaji maji salama hususani kwa wananchi wanaoishi jirani na migodi yake ya Bulyanhulu, Buzwagi na North Mara.
Akiwa ni msomi mwenye shahada katika masuala ya mahusiano ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Witwatersrand Afrika Kusini na taaluma za biashara, ualimu na uongozi, Senkondo anasema anajivunia kwa kupatiwa fursa ya uongozi na mwajiri wake.
Mbali ya elimu hizo, pia ana Stashahada ya Juu ya Usimamizi wa Biashara kutoka Chuo cha Elimu cha Biashara (CBE) na Stashahada ya Elimu ya Chuo cha Ualimu (TTC) cha Korogwe mkoani Tanga.
Anasema siku zote amekuwa akihakikisha anafanya kazi kwa weledi na kujiamini.
Anaeleza kuwa mafunzo mbalimbali aliyoyapata ndani ya kampuni tangu aajiriwe mwaka 2009, yamezidi kumjengea uwezo wa kufanya kazi zake kwa ufanisi zaidi.
Senkondo pia alisema anavutiwa na sera ya Barrick ya kutoa ajira na nafasi za uongozi bila ubaguzi wa kijinsia ambayo imewawezesha wanawake wengi kushikilia nafasi za uongozi katika sekta hii ya madini ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na mfumo dume.
Anasema kuondokana na changamoto ya kubaki nyuma ni muhimu watoto wa kike kupambana kusoma kwa bidii na wanapopata fursa kuzitumia vizuri ili kuondoa dhana kuwa wanawake hawana uwezo.
“Pia taasisi na makampuni yanapaswa kuwaamini wanawake na kuwapatia fursa za kuongoza ili waonyeshe uwezo kuwa wako sawa na wanaume au zaidi yao,” anaongeza Senkondo.
Anaeleza kuwa wanawake ambao wanajishughulisha na ujasiriamali, kilimo, ufugaji na shughuli nyinginezo wanapaswa kujiamini na kuendesha shughuli zao kwa ufanisi wakiwa na mtazamo wa kujikwamua kimaisha na kuacha utegemezi sambamba na kuboresha maisha yao.
Akiwa nje ya kazi, Senkondo anapenda kusoma vitabu, kuperuzi kwenye mitandao kwa ajili ya kupata taarifa mbalimbali na kukaa na familia yake.
Anatoa wito kwa wanawake wenzake popote walipo wazidi kujiendeleza kielimu na kujiamini na kuachana na dhana ya kufikiria kuwa wanaume wanao uwezo kuliko wanawake.
“Najua zipo changamoto nyingi zinatukabili kama wanawake, lakini vichwani mwetu tuondoe dhana kuwa tunapaswa kuwa nyuma ya wanaume kwa kila jambo, tukiondokana na dhana hiyo tutaweza kusonga mbele na ipo mifano ya wanawake hapa nchini wanaendelea kung’ara katika nafasi zao za kazi kuzidi hata wanaume na kufanya kwao vizuri kunatokana na elimu walizo nazo na kujiamini,” alisisitiza Senkondo.