10,100 waliositisha masomo warejeshwa shuleni

MOROGORO – Serikali imefanikiwa kuwarejesha shuleni nje ya mfumo rasmi wa elimu jumla ya wanafunzi wa kike elfu 10,100 katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2022 hadi 2024.

Idadi hiyo ya wanafunzi wengi ni waliokatisha masomo kwa kupata mimba na utoro, ambao wamerejeshwa shuleni kupitia vituo vya taasisi ya elimu ya watu wazima ikiwa ni miaka mitatu tu, tangu Serikali ilipotoa mwongozo maalum wa urejeshwaji wa wanafunzi hao.

Akifungua kikao cha utekelezaji wa shughuli za elimu maalum kwenye mikoa na halmashauri kilichowakutanisha maafisa elimu watu wazima ngazi ya mkoa na halmashauri nchi nzima mkoani Morogro, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Dk. Charles Msonde amesema hatua hiyo ni mafanikio makubwa katika historia ya nchi juu ya uboreshaji wa sekta ya elimu.

Advertisement

Kauli ya Dk. Msonde inakuja ili hali sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ikionesha kuwa asilimia 17 ya watanzania wote wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea hawajui kusoma wala kuandika.

Dk. Msonde amesema kutokana na hatua hiyo ndiyo maana Serikali ilielekeza idara zote za Elimu zisimame imara katika kuhakikisha utendaji kazi ngazi na idara mbalimbali unaimarishwa ili kutekeleza adhima ya serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha elimu inakuwa imara.

“Ni lazima tuimarishe Elimu ya watu wazima, elimu nje ya mfumo rasmi wa elimu, elimu ya msingi na elimu ya sekondari maana zote hizi ni elimu msingi na zikikaa kwa Pamoja, zikaimarika kwa Pamoja Watoto wakapata ujuzi na watu wazima wakapata ujuzi umahiri unaongezeka ndipo tunaposema sasa elimu imekuwa bora” alisema Dkt. Msonde.

SOMA: Usajili 2024: Fadlu Davis anukia Simba

Aliongeza kuwa “Na yeyote yule anayeanza kututenganishz idara tutamchukulia hatua, ndiyo maana nikasema tuitane wote hapa, tuwekeane mikakati, tupange ili tukitoka hapa tuhakikishe kwa vyovyote vile elimu inakuwa bora na tunasimamia vizuri utekelezaji katika sekta yetu.

Awali Mkurugenzi msaidizi wa elimu ya watu wazima OR – TAMISEMI Ernest Hinju amesema pamoja na masuala mengine lakini pia kikao hicho cha siku nne kitatoa fursa ya washiriki kupata uzoefu kutoka kwa wastaafu na wabobezi wa elimu ya watu wazima na elimu maalum pamoja na kufahamu wadau mbalimbali wanaojishughulisha na masuala mbalimbali ya elimu ya watu wazima na elimu maalum.