12 wadakwa kuvujisha mitihani

WATUMISHI wa  12 wa Baraza la Mitihani wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuvujisha mitihani ya kidato cha nne katika shule ya Sekondari ya Twiboki.

Aidha, walimu waliosimamia mitihani katika shule hiyo, barua zinaandikwa kwa waajiri wao ili hatua kali za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Hayo yamesemwa Bungeni leo Februari 9, 2023 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Adolf Mkenda akitolea ufafanuzi wa mwongozo uliyo ombwa na Mbunge wa Bunda Mwita Gitere  aliyetaka kufahamu watoto 66 waliofutiwa matokeo ya kidato cha nne katika shule ya Twiboki hatua gani zimechukuliwa kwa waliovujisha mitihani na wasimamizi wa mithiani hiyo.

“Hawa wasimamizi walisaini kuwa mitihani imefanyika vizuri na imemalizika salama je wamechukuliwa hatua gani? na kati ya wanafunzi 67 waliofanya mtihani mmoja tu ndio kapewa matokeo yake wengine 66 wamefutiwa inakuaje? alihoji Gitere

Akizungumzia suala hilo, Mkenda amesema “Ni vizuri wote tuwe makini  katika suala la mitihani na udanganyifu kwa ujumla wake, tunapozungumza ubora wa elimu ni pamoja na kuhakiki wale wanaofanya ‘transition’ kwa kuchujwa kupitia mitihani iwe inafanyika kwa ukweli.

“Madhara ya udanganyifu wa elimu ni makubwa kwenye mfumo wote wa elimu, kwenye uchumi wetu na hata maisha yetu….; “Ukaja ukakuta daktari ambae kapita kwa magumashi kwa kudanganyifu  alafu akamtibu mwanao, madhara yake ni makubwa sana hivyo tuna umakini sana wa kufuatilia katika mitihani.

Mkenda, amesema kilichotokea katika shule hiyo ya Twiboki iliyopo mkoani Mara ni kwamba kuna sababu za kutosha kulikuwa na udanganyifu katika mitihani, majibu yanafanana ambayo ‘statistically’ haiwezekani yakafanana

“Kama wizara tumehakiki, swali la msingi kama ni hivyo kulikuwa na watu wanasimamia iwezekanaje wawe na majibu yanayofanana bila ‘coordination’ ni hatua gani inachukuliwa?  Mbona mmoja matokeo yake yametangazwa wengine wote hawakutangazwa?

“Hatua zilizochukuliwa nimepewa taarifa jana kuwa  watu 12 wapo mahabusu kwa sababu za kuvujisha mitihani na hao wapo na connection na shule hii ya Mara. Na uchunguzi unaendelea kujua nini kilitokea mpaka wanafunzi wakawa na majibu yanayofanana.”Amesema Mkenda na kuongeza

“Pili barua zinaandikwa kwa mamlaka kwa wale waliosimamia mtihani wachukuliwe hatua zaidi za kisheria.

Mkenda amesema pia wapo kwenye uchunguzi wa shule ambayo imefungua kabrasha za mitihani mapema kabla ya muda na kujibu maswali na wanafunzi katika Bwalo la Chakula na badae ndio wakawaingiza katika vyumba vya mitihani.

“Sasa hili la mtoto mmoja ambaye amepewa matokeo yake hatujui kama hakuonyeshwa mtihani au alionyeshwa akafanya kwa njia anazozijua yeye, tupo tayari kukutana na wazzi kama wanahisi Watoto wao wameonewa.

Nae Spika wa Bunge, Tulia Ackoson amesema kuwa hakuna maana ya kutetea udanganyifu na haupaswi kuvumilika.

“Nafasi tulizonazo leo ndio watakuja kuzikalia kesho, wanafunzi hawana namna ya kupata mitihani bila kuwezeshwa, mnyororo mzima uliohusika uchukuliwe hatua.”Amesema Tulia.

Katika matokeo ya shule hiyo yaliyochapishwa katika tovuti ya Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) yanaonyesha wanafunzi 67 ndiyo waliosajiliwa na kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka jana.

Athumani Amas ambaye ni Kaimu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), amekaririwa akisema kuwa kati ya wanafunzi hao, 66 wamefutiwa matokeo kwa sababu wamefanya udanganyifu.

Kwa mujibu wa Necta, ni mwanafunzi mmoja tu mwenye matokeo aliyepata daraja la kwanza la pointi nane.

Wanafunzi hao 66 waliofutiwa matokeo ni sawa na asilimia 20 ya wanafunzi 333 ambao wamefutiwa matokeo katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2022.

Hiyo ni sawa na kusema kwa kila wanafunzi 10 waliofutiwa matokeo, wawili wanatoka katika shule hiyo iliyopo Kanda ya Ziwa.

Watahiniwa hao waliofutiwa matokeo kutokana na udanganyifu wanaweza kufanya tena mtihani wa kidato cha nne kama watahiniwa binafsi kwa kutumia namba zao walizopata mwaka 2022.

Habari Zifananazo

Back to top button