15 wafanyiwa upasuaji umeme wa moyo

JUMLA ya wagonjwa 15 wenye matatizo katika mfumo wa umeme wa moyo, wamefanyiwa upasuaji na wengine kuwekewa betri  kwa siku tano katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), ambapo kiasi cha Sh Milioni 493 kimeokolewa kutokana na huduma hiyo kutolewa ndani ya nchi.

Gharama ya matibabu kwa wagonjwa 15 ni Sh milioni 253,  lakini kama wangepelekwa nje ya nchi kama  India au Afrika Kusini ingegharimu  Sh  milioni 746.

Kambi hiyo ya matibabu ilianza Aprili 24 hadi jana ambapo madaktari wa JKCI walishirikiana na Madaktari kutoka Marekani.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, daktari bingwa wa moyo,Yona Gandiye alisema matarajio yao ilikuwa kuhudumia wagonjwa 10 lakini kadiri walivyoendelea wamehudumia 15 kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo.

Dk Gandiye amebainisha kuwa  kati ya hao wagonjwa  sita wamewekewa betri ya moyo,wawili wamebadilishiwa vifaa vilivyokuwa vimeisha muda ,wagonjwa wawili waliwekewa kifaa kinaitwa CRTD kutokana na upande wa kushoto kushindwa kufanya kazi.

“Wagonjwa sita walipata mapigo ya moyo kwa haraka kwa kutumia mitambo tuliweza kuwatibu na hawatapata tena ile hali,” amesema.

Amesema mtambo mpya uliofungwa una uwezo wa kuwasaidia kusoma namna mtiririko wa mapigo ya moyo yanavyotoka ndani ya moyo hasa wale wagonjwa wanaolalamika kuzimia,moyo kwenda haraka sana wakiwa wanafanya kazi na wakabaini tatizo linatoka wapi.

“Aina hiyo ya mashine inaitwa covetion kwa maana tulikuwa tunategemea zaidi namna mapigo yanavyotiririka,”ameeleza.

Aidha amebainisha kuwa tatizo la uzalishaji wa mapigo ya moyo inaweza kutokea kutokana na sababu mbalimbali, kwanza muhusika kuzaliwa na tatizo la kuzalisha mapigo ya haraka au ya chini na wanawekewa vifaa maalum, ili kuongeza mapigo.

Pili ameainisha kuwa mtu anapokuwa na presha mapigo yanaenda haraka na tatu sababu ambazo haijulikani.

“Tunaishukuru serikali kwa kutupatia mashine hii ya kugundua mwenendo wa mapigo ya moyo na mashine kubwa pia ilinunuliwa na ina uwezo mkubwa, dakatari muda wowote anaweza kutoa taswira na umbile la moyo na kugundua hitilafu iko sehemu gani na tunashughulikia sehemu husika,”amefafanua na kuongeza:

Habari Zifananazo

Back to top button