219,321 kuboresha taarifa Kagera
TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imefanya mkutano wake na wadau wa uchaguzi kujadili uboreshaji wa Daftari la kudumu la wapiga Kura ambapo mkoa wa Kagera zoezi la kuboresha daftari hilo litaanza August 8 Hadi 11 mwaka huu.
Kupitia mkutano huo Makamu Mwenyekiti wa INEC, Jaji wa Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk ametoa wito kwa wadau kuhakikisha wanahamasisha wananchi wote wenye sifa za kujiandikisha katika Daftari la kudumu kujitokeza kwa wingi ili kushiriki katika chaguzi na kutimiza matakwa yao ya msingi katika kuchagua viongozi.

“Wadau wetu wengine ni viongozi wa vyama vyote vya siasa kutokana na mabadiliko ya sheria za uchaguzi mwaka huu tumeona katika vituo vyetu kila kiongozi wa chama cha siasa anaweza kuweka wakala katika kituo cha kuandikisha ili kuona kama kila Mtanzania anapata haki ya kuandikwa na hakuna mtu kutoka nje ya Tanzania anayeandikwa ,tunaomba mawakala wa vyama wawepo,”amesema Mbarouk.

Akizunumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Uchaguzi, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Giveness Aswile amesema mkoa wa Kagera unatarajia kuwa na ongezeko vituo vya kuboresha daftari 101 na kufanya vituo vya uboreshaji kufikia 1,778.
SOMA: Uboreshaji daftari wapiga kura kuzinduliwa leo
Aidha mkoa huo utakuwa na ongezeko la wanaotarajia kuboreshewa taarifa zao wapya wapatao 219,321 sawa na asilimia 15 hivyo kufanya idadi ya wenye sifa katika Daftari la kudumu la wapiga kura kuwa 1,631,329 ukilinganisha na uboreshaji uliopita ambao ulikuwa na taarifa za wananchi 1,412,018 mkoani Kagera.

Amesema watanzania pekee ndio wenye sifa za kujiandikisha wenye umri wa miaka 18, waliozaliwa kabla ya Octoba 2007 wakiwemo wafungwa wenye kifungo cha miezi 6 huku akitoa wito kwa waandikishaji kuhakikisha wanatoa kipaumbele kwa makundi maalumu kama watu wenye ulemavu na wazee kuandikishwa haraka.
Akizundua uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura katika uwanja wa Kawawa, mkoani Kigoma Julai 20. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 jumla ya wapiga kura wapya 5,586,433 wataandikishwa katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Alisema wapiga kura hao ni ambao watakuwa wametimiza umri wa miaka 18 katika kipindi cha kuanzia mwaka 2020 baada ya uchaguzi mkuu uliopita na ambao watatimiza umri huo ifikapo tarehe ya uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2025.

Uzinduzi huo uliashiria kuanza kwa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura nchi nzima ambapo Mikoa iliyoanza uboreshaji wa daftari hilo Julai 20, 2024 hadi Julai 26, 2024 ni Kigoma, Katavi na Tabora.
Majaliwa alisema kwa mujibu wa taarifa za Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, inakadiriwa kuwa wapiga kura 4,369,531 wataboresha taarifa zao.
“Idadi hii si ndogo kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura hivyo nitoe rai kwa kila mpiga kura aliyeandikishwa na mwenye uhitaji wa kuboresha taarifa asisite katika vituo vya kujiandikisha tume imejipanga kuhakikisha wananchi wote wanafikiwa popote walipo mpaka vitongojini”



