TCU kushusha rungu kwa vyuo vitakavyokaidi maelekezo

DAR ES SALAAM: TUME  ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetoa maelekezo yanayopaswa kufuatwa kwa vyuo vya elimu ya juu na waombaji wapya katika mchakato wa udahili unaondelea kwa sasa.

TCU imesema haitasita kuchukua hatua kwa vyuo ambavyo vitakwamisha waombaji wa vyuo kushindwa kufanya udahili kwa vyuo wanavyotaka.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Mtendaji Tume ya vyuo vikuu Tanzania (TCU,) Profesa Charles Kihampa akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam.

Prof Kihampa amezitaka taasisi za elimu ya juu kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika zoezi la udahili ili kuepusha usumbufu usiokuwa na lazima kwa waombaji wa udahili.

Amewataka waombaji kusoma miongozo ya sifa ya kujiunga na programu husika, ili kuona wanakidhi vigezo kabla ya kutuma maombi ya udahili.

Amewataka waombaji wenye changamoto ya kupokea namba za siri ya uthibitishaji katika chuo kimoja, kuingia kwenye mifumo ya udahili wa vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa namba maalum ya siri ili kuweza kuthibitisha katika chuo husika.

Amesema pia waombaji wanashauriwa kutumia barua pepe au mitandao ya simu na udahili ufanyike kupitia akaunti ambayo muombaji alitumia kuomba udahili mwanzoni.

“Taasisi zote za elimu ya juu zinazofanya udahili ziruhusu waombaji kuingia katika mifumo yao na kuwapa namba ya siri ili wafanya udahili na kuthibitisha wao wenyewe,” amesema.

Amesema pia taasisi za elimu ya juu zihakikishe waombaji udahili wanajithibitisha wao wenyewe kupitia akaunti zao na si vinginevyo na wanaotaka kubadili uthibitisho waingie katika akaunti za vyuo, ili wajithibitishe katika chuo kingine.

“Waomba wanaotaka kubadili maombi wafute maombi ya awali na kutuma mapya na vyuo vinatakiwa kutoa elimu kwa umma namna sahihi ya kuwasiliana na vyuo husika ili kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza,” amesema.

Pia Prof Kihampa ameongeza zoezi la kutuma maombi ya udahili kwa wanafunzi waliopata chuo zaidi ya kimoja linaenda vizuri ambapo hadi jana jumla ya waombaji 23,387 wamethibitisha kati ya 43,213 wanaopaswa kufanya hivyo.

Kihampa amewataka waombaji ambao hawajathibitisha wakamilishe uthibitisho wao kupitia akaunti zao kwenye vyuo wanavyopenda na kwamba hakuna mwanafunzi atakayekosa chuo kwa kushindwa kuthibitisha.

Amefafanua kuhusu taarifa za vyuo kushiriki kukwamisha waombaji kujidahili katika vyuo wanavyotaka Kihampa alisema TCU imejipanga kuhakikisha waombaji wote wanapata udahili bila kukwamishwa na mtu yoyote.

Kihampa amesema jukumu la vyuo ni kushirikiana na wanafunzi ambao wanataka kufanya udahili wa kujiunga na vyuo vyao na si vinginevyo.

“TCU tupo makini sana katika mchakato wa udahili ambao unatumia mifumo zaidi, hatutasita kuchukua hatua kwa chuo ambacho kitabainika kukwamisha wanafunzi kufanya udahili kwenye chuo anachokitaka,” amesema.

Amesema hakuna muombaji wa udahili ambaye atanyimwa fursa ya kuchagua chuo anachokitaka, iwapo ataweza kushindana na ushindani wa chuo husika na kuwataka watakaokwamishwa wawasiliane na TCU.

Prof. Kihampa amesema zipo changamoto za waombaji kuwa wapya, ila isitokee chuo kushiriki kukwamisha maombi ya mwanafunzi.

“Yoyote ambaye amepata udahili katika vyuo zaidi ya kimoja ana uhuru wa kufanya udahili kwenye chuo anachokitaka na isitokee kukwamishwa na mtu yoyote,” amesisitiza.

Habari Zifananazo

Back to top button