400 kupatiwa matibabu ya macho Mbarali

ZAIDI ya watu 400 wenye matatizo ya macho wanatarajiwa kupatiwa matibabu, ikiwemo ya upasuaji wa mtoto wa jicho katika kambi ya siku 10 itakayofanyika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali.

Kaimu Meneja wa Mpango wa Taifa wa huduma za Macho kutoka Wizara ya Afya, Dk Greater Mande amesema kuwa kambi hiyo inayoendeshwa na Wizara ya Afya kupitia watoa huduma kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda-Mbeya na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mbeya kwa kushirikiana na  Shirika la Hellen  Keller International.

Amesema mradi huu wa upasuaji wa mtoto wa jicho utatekelezwa kwa muda wa mwaka mmoja wilayani humo na mpaka kumalizika kwa mradi huo,  watu wapatao 900 wanatarajiwa kufanyiwa upasuaji.

“Ulemavu wa kutokuona haukubaliki, kwani zipo njia za kuzuia na kutibu zikiwemo za gharama nafuu, hivyo nawasihi wakazi wa Mbarali kujitokeza kwa wingi kwani huduma hizi tembezi zimewafikia na hazina gharama yeyote,” amesema.

Amesema shirika hilo linatumia njia ya kuwaibua wagonjwa kwa kupita nyumba kwa nyumba kwa hatua ya awali na baadae kuwafikisha kwenye kituo cha kutolea huduma kwa ajili ya upasuaji.

Naye Meneja Mradi wa Shirika la Hellen Keller International, Athuman Tawakal amesema kambi hiyo ni ya kwanza katika wilaya ya Mbarali na wanatarajia kuwafikia watu takriban 900 kutoka vitongoji vyote.

Habari Zifananazo

Back to top button