Waandishi epukeni taarifa za uongo

DAR-ES-SALAAM : WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuwa makini katika kuripoti taarifa za uchaguzi, hususan katika zama za teknolojia ya akili bandia (AI) ambazo zimeongeza kasi ya usambazaji wa taarifa potofu, chuki na uchochezi mitandaoni.

Wito huo umetolewa katika warsha ya siku mbili iliyoandaliwa na Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kwa kushirikiana na mpango wa #defyhatenow kupitia Global Action for Peacebuilding (GAPI) na kufadhiliwa na GIZ.

Warsha hiyo imewaleta pamoja waandishi mbalimbali na kuwapa mafunzo kuhusu fact-checking, usalama wa habari mtandaoni, matumizi salama ya AI na mbinu za kuandika taarifa zinazojenga amani wakati wa uchaguzi.

Njokii Kariuki kutoka Global Peace Initiative, Nairobi, Kenya, amesema baadhi ya taarifa huundwa kwa makusudi ili kuchochea hisia, kuharibu sifa za watu au taasisi, hasa wakati wa uchaguzi.

“Waandishi wanapaswa kuchunguza taarifa kwa kina kabla ya kuchapisha. Waulize: nani alisema, lini, kwa muktadha upi na kwa lengo gani?” alisema Kariuki.

Kwa upande wake, Silvia Daulinge kutoka TAMWA amesema waandishi wanakabiliwa na changamoto kubwa kutokana na kasi ya kusambaa kwa taarifa zisizo sahihi kwenye mitandao ya kijamii na hata vyombo vya habari rasmi.

“Kumekuwa na ongezeko la hotuba za chuki na udhalilishaji, hasa dhidi ya wanawake wanaogombea nafasi za uongozi. Wanawake, vijana na makundi maalumu wana haki ya kushiriki bila kuonewa au kudhalilishwa,” alisema.

Florence Majani kutoka TAMWA aliwataka waandishi kutumia taaluma yao kujenga mshikamano wa kijamii na kulinda demokrasia. “Tumieni  kalamu zenu kujenga jamii yenye mshikamano, kuheshimu haki na usawa,” alisema.

Warsha hiyo imeelezwa kuwa muhimu wakati huu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025, ambapo vyombo vya habari vinatarajiwa kuwa mhimili wa  na chanzo cha taarifa sahihi. SOMA: Uchaguzi Mkuu kugharamiwa na fedha za ndani

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button