Wadau wa misitu wafundwa

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja amewaasa wadau wa misitu kote nchini washiriki kikamilifu katika usimamizi na utunzaji wa maeneo ya misitu ya vijiji ili kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi.

Ameyasema hayo leo Novemba 15, 2022 wakati wa ufunguzi wa warsha ya 22 ya Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania (MJUMITA)mkoani Morogoro.

“Kasimamieni misitu vizuri msigawe maeneo hovyo, mkaweke mpango wa matumizi bora ya ardhi ili kuzuia uvamizi kwenye maeneo ya hifadhi.”Amesema  Masanja

Advertisement

Aidha, amewataka viongozi wa MJUMITA kuwaelimisha wananchi juu ya usimamizi wa misitu na umuhimu wa uhifadhi.

Aidha, amesisitiza kuwa misitu ikisimamiwa vizuri ina uwezo mkubwa wa kudhibiti mabadiliko ya tabia ya nchi, kutunza vyanzo vya maji, kuwa makazi ya wanyama hai na chanzo cha mapato kwa jamii hasa kwa kutekeleza shughuli za ufugaji nyuki.

Lengo la warsha hiyo ni kujenga uelewa wa pamoja wa dhana za ujumuishi wa wanawake na vijana katika uhifadhi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi, kubadilishana uzoefu wa namna ya kutekeleza dhana ya ushiriki wa jinsia kwenye uhifadhi wa misitu, kujadiliana kuhusu fursa na changamoto zinazowakabili wanawake na vijana katika uhifadhi na ushiriki katika mnyororo wa thamani ya mazao ya misitu.