Rais Mwinyi azindua Mji wa Dk. Hussein Mwinyi

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ameuzindua rasmi Mji wa Dk. Hussein Mwinyi uliopo Mombasa, Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF) kuendelea kujikita katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo yenye tija kwa Taifa.
Rais Dk. Mwinyi ametoa kauli hiyo leo, Desemba 23, 2025, wakati wa uzinduzi wa mji huo wa kisasa uliofanyika katika kuadhimisha Miaka 62 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Amesema mifuko ya hifadhi ya jamii imekuwa nguzo muhimu ya maendeleo katika nchi nyingi duniani, huku akiipongeza ZSSF kwa kuanza vyema utekelezaji wa mradi huo mkubwa, hususan katika ujenzi wa makazi ya kisasa na ya gharama nafuu kwa wananchi.
Aidha, ameitaka ZSSF kuongeza wigo wa uwekezaji kwa kujikita zaidi katika miradi mikubwa ikiwemo miradi ya uzalishaji na usambazaji wa nishati ya umeme, baada ya mafanikio iliyoyapata katika ujenzi wa masoko, vituo vya mabasi na nyumba za makazi.

Rais Dk. Mwinyi amesema Zanzibar inahitaji kuwa na miji mipya ya kisasa yenye hadhi na ubora ili kuwawezesha wananchi kuishi katika mazingira bora na salama. Ameeleza kuwa bado wapo wananchi wengi wanaoishi katika makazi duni na maeneo yasiyopimwa, hali inayosababisha changamoto za kimazingira na upangaji wa miji. SOMA: Mwinyi Azindua Miradi ya Maendeleo Zanzibar
Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kuunga mkono juhudi za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuboresha maisha yao. Sambamba na uzinduzi wa mji huo, Rais Dk. Mwinyi pia amezindua nyumba za gharama nafuu pamoja na msikiti mpya uliojengwa katika eneo hilo ujulikanao kama Masjid Balad Salaam.

Ameitaka ZSSF kwa kushirikiana na wakaazi wa Mji wa Dk. Hussein Mwinyi kuhakikisha wanazitunza nyumba hizo ili ziendelee kuwa na haiba na ubora kwa muda mrefu. Vilevile, Rais Dk. Mwinyi ameridhia ombi la ZSSF la kupatiwa eneo kwa ajili ya ujenzi wa ofisi katika Mji wa Serikali Kisakasaka, na kuiagiza Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi kuipatia taasisi hiyo eneo la ardhi kwa ajili ya ujenzi huo, huku akisisitiza ofisi zitakazojengwa ziwe bora na za mfano.



