Maofisa elimu waagizwa kuandaa kanzidata sahihi

ARUSHA: Maofisa elimu wa mikoa na halmashauri zote nchini wameagizwa kuhakikisha wanakuwa na kanzidata sahihi katika kila halmashauri ili kuiwezesha serikali kupanga kwa ufanisi rasilimali watu, madarasa na vifaa mbalimbali vya shule.

Lengo ni kuondoa changamoto ya upungufu wa miundombinu ifikapo mwaka 2028, wakati wanafunzi wa darasa la sita na la saba watakapohitimu kwa pamoja.

Aidha, Wakuu wa mikoa wote nchini wameagizwa kuzisimamia halmashauri zao kuhakikisha zinaweka siku maalum ya kusikiliza malalamiko na kero za wananchi katika ngazi ya kata, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kupatikana kwa ufumbuzi wa changamoto zinazowakabili wananchi katika ngazi ya chini.

Maagizo hayo yametolewa jijini Arusha na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Riziki Shemdoe, wakati akifungua kikao cha Umoja wa Maofisa Elimu wa Mikoa na Halmashauri (REDEOA).

Amesema ili serikali isiweze kukumbwa na changamoto ya uhaba wa madarasa, matundu ya vyoo na vifaa vingine muhimu, ni lazima maofisa hao waandae kanzidata sahihi zitakazosaidia mipango madhubuti kwa ajili ya wanafunzi watakaohitimu darasa la sita na la saba kwa pamoja mwaka 2028.

“Hatutaki kusikia mwaka 2028 watoto wanashindwa kuendelea na masomo kwa sababu ya ukosefu wa madarasa, vyoo au huduma nyingine muhimu,hakikisheni mnatoa taarifa sahihi zitakazoiwezesha serikali kujipanga vizuri,vilevile, wakuu wa mikoa simamieni wakurugenzi wasikilize kero za wananchi katika kila kata, mkiona wananchi wanalalamika wakati wa ziara za viongozi, mjue kero zao hazikusikilizwa kwa wakati,”

Profesa Shemdoe amesisitiza umuhimu wa wakurugenzi wa halmashauri pamoja na Timu za Usimamizi wa Halmashauri (CMT) kuwa karibu na wananchi na kushughulikia changamoto zao mapema, badala ya kusubiri zibainike wakati wa ziara za viongozi wa kitaifa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button