Samia Ardhi Kliniki yawafikia wanawake Simiyu

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesogeza karibu huduma za sekta ya ardhi kwa wanawake nchini kupitia Kliniki Maalumu ya Ardhi ijulikanayo kama Samia Ardhi Kliniki.
Kliniki hiyo inaendeshwa katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo Mkoa wa Simiyu ni miongoni mwa mikoa inayotekeleza huduma hiyo. Inatarajiwa kuzinduliwa rasmi Machi 4, 2026 na Mkuu wa Mkoa huo, Anamringi Macha, katika Viwanja vya Sabasaba vilivyopo Bariadi. SOMA: Wakazi zaidi ya 400 Ilemela kunufaika kliniki ya ardhi

Katika kufanikisha kliniki hiyo, Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Simiyu pamoja na wataalamu wa sheria kutoka Mama Samia Legal Aid wanatoa huduma mbalimbali za sekta ya ardhi. Huduma hizo ni pamoja na upimaji wa ardhi, utoaji wa hati miliki, uhamishaji wa umiliki, uthamini wa ardhi, kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi katika sekta ya ardhi na kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu matumizi bora ya ardhi.
Kliniki hiyo inalenga kutoa huduma za ardhi kwa wanawake nchini kote kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake, yatakayofanyika kuanzia Machi 2 hadi 7, 2026, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Haki sawa kwa wanawake na wasichana; Msingi jumuishi kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”



