Ayoub ahimiza ufanisi huduma zimamoto

MWANZA: Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahomud amewahimiza askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kuongeza uwajibikaji katika utoaji huduma kwa kufika kwa wakati katika maeneo ya matukio.
 
Amesema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuboresha miundombinu na vitendea kazi ili kuongeza ufanisi wa jeshi hilo.
 
Naibu Waziri Ayoub ameyasema hayo leo, katika kikao cha Baraza Dogo la Wafanyakazi wa jeshi hilo jijini Mwanza ambapo amewaeleza kuwa viongozi wa wizara wana imani na matumaini makubwa kwa askari wa jeshi hilo katika kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo na weledi.
 
Aidha, amewataka kutumia baraza hilo kutathmini mafanikio na changamoto zilizopo ili kuimarisha zaidi utekelezaji wa majukumu yao kisheria na kitaaluma.
 
Naye, Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, John Masunga amebainisha kuwa jeshi hilo lina jumla ya vituo 80 vya Zimamoto na Uokoaji katika mikoa yote ya Tanzania Bara, ambapo 58 vipo katika ngazi ya Wilaya na 22 katika viwanja vya ndege.
 
Aidha, jeshi lina ofisi 73 za kutoa elimu ya kinga na tahadhari ya majanga ya moto pamoja na vituo saba vya huduma mipakani, huku likiwa na uhitaji wa vituo vipya 237 ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
 
Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Fedha Mbaraka Semwanza, kwa niaba ya wafanyakazi wenzake ameahidi kuwa wataendelea kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo, huku wakihakikisha vitendea kazi vilivyopatikana vinatunzwa na kutumika ipasavyo katika kuokoa maisha na mali za wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button