Tanzania yashiriki mkutano wa uchukuzi Afrika Kusini

JOHANNESBURG: Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, ameshiriki Mkutano wa Kimataifa wa Masuala ya Uchukuzi (NCT) uliofanyika katika ukumbi wa Gallagher Estate jijini Johannesburg, Afrika Kusini. Mkutano huo ulifunguliwa rasmi na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa.

Sambamba na ushiriki huo, Kihenzile pia alishiriki mjadala wa mawaziri wa uchukuzi uliokuwa na mada isemayo: “Uongozi na Utawala katika Utekelezaji wa Mfumo Jumuishi, Endelevu na Salama wa Uchukuzi unaochochea Ukuaji Jumuishi wa Uchumi, Uhifadhi wa Ajira na Maendeleo ya Jamii Kusini mwa Afrika.”

Katika mjadala huo, Naibu Waziri amewasilisha hatua mbalimbali zilizofikiwa na Tanzania katika kuendeleza miundombinu ya uchukuzi, ikiwemo uwekezaji mkubwa katika reli ya kisasa (SGR), maboresho ya bandari, viwanja vya ndege pamoja na miundombinu ya barabara.

Aidha, ameeleza kuwa Serikali ya Tanzania inaendelea kuweka mazingira rafiki kwa uwekezaji na kuwakaribisha wawekezaji kushiriki katika miradi mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya uchukuzi. Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha biashara, kuongeza ushindani wa kiuchumi, na kukuza maendeleo ya kikanda.




