Kikwete aanza vyema juhudi za amani Sudan Kusini

JUBA — Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, ameanza kuhuisha mchakato wa amani nchini Sudan Kusini baada ya kukamilisha ziara ya siku mbili jijini Juba.
Akiwa Mwakilishi Maalum wa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika kwa Ukanda wa Pembe ya Afrika na Bahari ya Shamu, Kikwete alikutana na Rais Salva Kiir pamoja na viongozi wengine wa serikali kujadili utekelezaji wa makubaliano ya amani ya mwaka 2018 (R-ARCSS).
Rais Kiir alimhakikishia kuwa mchakato wa amani unaendelea, huku akisisitiza dhamira ya serikali kuandaa uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Desemba 2026 bila kuahirishwa tena. Pia alieleza juhudi za kuimarisha mazungumzo jumuishi kati ya pande mbalimbali za kisiasa.
Mbali na serikali, Kikwete alikutana na vyama vya siasa, asasi za kiraia, viongozi wa dini na wanataaluma, akilenga kuhakikisha ushirikishwaji mpana katika mchakato wa amani.
Mwanaharakati wa kiraia Edmund Yakani alimpongeza Kikwete, akieleza kuwa uzoefu wake katika upatanishi unatoa matumaini ya kufanikisha mazungumzo jumuishi yatakayowaleta pamoja wadau wote, ndani na nje ya nchi.

Kikwete pia alikutana na wadau wa kimataifa wakiwemo IGAD, UNMISS na RJMEC, pamoja na mabalozi kutoka nchi mbalimbali, ili kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika mchakato huo.
Ziara hiyo inaongeza matumaini ya kuimarika kwa hali ya kisiasa nchini South Sudan, wakati nchi hiyo ikijiandaa kuelekea uchaguzi muhimu wa mwaka 2026.



