Mpogolo awapiga mkwara makandarasi Ilala

DAR ES SALAAM: MKUU wa Wilaya ya Ilala, mkoani Dar es Salaam, Edward Mpogolo, ametoa onyo kali kwa wakandarasi wote wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara wilayani humo, akiwataka kuzingatia mikataba na kukamilisha kazi kwa wakati.

Mpogolo alitoa onyo hilo wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi mbalimbali ya barabara, aliyoifanya kwa kushirikiana na baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, ambapo alitembelea miradi inayotekelezwa na wakandarasi, wengi wao wakiwa makampuni ya wazawa.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mpogolo aliwakosoa baadhi ya wakandarasi kwa kuchelewesha miradi kwa visingizio visivyo na msingi, hali inayosababisha usumbufu kwa wananchi huku Serikali ikiwa tayari imeshatoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa kazi hizo.

Pia, alionya tabia ya baadhi ya wakandarasi kukaidi maelekezo ya wasimamizi wa miradi kutoka TARURA na TANROADS, wakitumia mwanya wa kufahamiana na baadhi ya viongozi wa juu. Alisisitiza kuwa vitendo hivyo havitavumiliwa, hasa pale vinapoambatana na ujenzi wa barabara chini ya viwango vilivyokubaliwa kwenye mikataba.

Mpogolo, pia alieleza wasiwasi wake juu ya wakandarasi wanaochukua miradi mingi kwa wakati mmoja bila kuwa na uwezo wa kutosha wa rasilimali na vifaa, jambo linalosababisha baadhi yao kutelekeza miradi au kuchelewesha utekelezaji wake.

Kutokana na hali hiyo, aliagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uchunguzi wa miradi kuchukua hatua kali dhidi ya wakandarasi wanaokiuka taratibu na kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika Wilaya ya Ilala.

Katika ziara hiyo, Mpogolo, alitaja baadhi ya barabara zilizokaguliwa kuwa ni pamoja na Halisi na Kimanga, zilizogharimu Sh bilioni 1.7 zilizotolewa mwaka 2024.

Barabara nyingine ni Mafia, Masasi, Magila, Bondi na Muhonda, zilizogharimu Sh bilioni 1.8 zilizotolewa mwaka 2025.

Pamoja na barabara za Mwanza, Livingstone, Nyamwezi, Kipati, Msikitini, Sharifushamba, Kigoma na Tunduru, zilizogharimu Sh bilioni 1.9.

Mpogolo alisisitiza kuwa Serikali haitavumilia uzembe wowote utakaoathiri ubora na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha miundombinu na maisha ya wananchi.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button