EACOP yatekeleza programu ya kujenga uwezo kukuza ushiriki wa wazawa

DODOMA: JITIHADA za kukuza ushiriki wa wazawa kwenye Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) zimeendelea kuimarika, baada ya kuzinduliwa kwa mpango maalumu wa kuwajengea uwezo Watanzania kushiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo sekta ya mafuta na gesi.

Mpango huo wa mafunzo ya kitaalamu ya uchomeleaji wa kisasa kwa kutumia teknolojia ya “Orbital Welding” umezinduliwa rasmi leo katika Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Dodoma.

Programu hiyo ya kiufundi yenye viwango vya hali ya juu inalenga kuwajengea uwezo wachomeleaji 30 wa Kitanzania kwa kuwapatia ujuzi wa kimataifa utakaowawezesha kushindana katika sekta ya nishati na miundombinu duniani.

Mafunzo hayo yanafadhiliwa na EACOP kwa kushirikiana na VETA pamoja na kampuni ya Panyu Chu Kong Steel Pipe (Zhuhai) Co., Ltd (PCK), ambayo ni miongoni mwa wazalishaji wakubwa wa mabomba ya mradi wa EACOP.

Kupitia mpango huo, washiriki 30 wanatarajiwa kuthibitishwa kwa viwango vya kimataifa vya uchomeleaji.

Mpango huu unaendana na dira ya EACOP ya kukuza ushiriki wa wazawa kwa lengo la kuimarisha ukuaji wa uchumi na maendeleo ya viwanda nchini kupitia kuongeza ujuzi kwa Watanzania.

Uzinduzi huo uliongozwa na viongozi kutoka EACOP wakiongozwa na Mkuu wa Mafunzo na Ujenzi wa Uwezo wa Ushiriki wa Wazawa, Martha Makoi, pamoja na viongozi waandamizi wa VETA.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Makoi alisema programu hiyo ni sehemu muhimu ya utekelezaji wa mkakati wa EACOP wa kuacha urithi wa kitaalamu wa kudumu nchini Tanzania.

“Kwa kuwapatia washiriki hawa vyeti vya viwango vya kimataifa vya uchomeleaji, hatujengi bomba la mafuta pekee, bali tunajenga nguvu kazi ya Kitanzania yenye ushindani wa kimataifa,” alisema.

Alieleza kuwa teknolojia ya “orbital welding” ni muhimu katika mifumo ya shinikizo kubwa na miundombinu nyeti, hivyo kuwapo kwa wataalamu wazawa wenye uwezo wa kutumia teknolojia hiyo ni hatua muhimu kwa maendeleo ya viwanda nchini.

Baada ya kukamilika kwa mafunzo hayo, washiriki watapata vyeti vya kimataifa vitakavyowawezesha kufanya kazi katika miradi mikubwa ndani na nje ya nchi.

Programu hiyo inaendeshwa na mtaalamu wa kimataifa wa uchomeleaji (International Welding Engineer-IWE) na inatekelezwa na Shirika la Small Enterprise Supplier Development Corporation (SESDCorp), ambalo lina uzoefu katika kuendeleza ujuzi na ushiriki wa wazawa nchini.

Mafunzo hayo yaliyozinduliwa leo yanatarajiwa kuendelea hadi Juni 21 mwaka huu na yanaonekana kuwa hatua muhimu katika kuifanya Tanzania kujitegemea katika sekta maalumu ya uhandisi na teknolojia za kisasa.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button