Mabaraza ya usuluhishi yatakiwa kutanguliza maridhiano

KAGERA: Utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala (ADR) umeendelea kutajwa kuwa suluhisho muhimu katika kuimarisha amani na mshikamano katika familia na jamii, huku wananchi wakihimizwa kutumia njia za mazungumzo na usuluhishi badala ya kufikishana mahakamani kwa migogoro inayoweza kumalizwa kwa njia ya maridhiano.

Hayo yamewekwa wazi katika mafunzo ya kuyajengea uwezo mabaraza ya Usuluhishi wa Ndoa kutoka Wilaya ya Ngara mkoani Kagera iliyoratibiwa na Wizara ya Katiba na Sheria.

Akifungua mafunzo hayo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngara, Teofilda Gota William, amesema kuwa Mabaraza ya Usuluhishi yana nafasi kubwa katika kulinda maadili ya jamii na kudumisha utulivu wa familia nyingi zinazokabiliwa na changamoto za ndoa na migogoro ya kifamilia.

Amesema kuwa Serikali inaendelea kuthamini mchango wa mabaraza hayo kwa kuwa yanasaidia kupunguza mzigo wa mashauri mahakamani na kuwapa wananchi nafasi ya kupata suluhu kwa haraka, gharama nafuu na kwa kuzingatia utu na heshima ya wahusika.

Aidha, amewataka wajumbe wa mabaraza ya usuluhishi kufanya kazi kwa weledi, haki na uadilifu ili kuhakikisha kila mwananchi anayefika mbele yao anapata nafasi ya kusikilizwa kwa usawa bila upendeleo wowote.

Amesisitiza kuwa migogoro mingi ya ndoa inaweza kumalizika kwa maelewano ikiwa usikivu na hekima vitatumika ipasavyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala (ADR), kutoka Wizara ya Katiba na Sheria Felix Chakila amesema kuwa, matumizi ya njia mbadala za utatuzi wa migogoro yamekuwa yakisaidia kujenga mahusiano bora katika jamii na kurejesha amani kati ya pande zinazohasimiana.

Chakila ameeleza kuwa usuluhishi wa ndoa unahitaji busara, uvumilivu na uwezo wa kusikiliza pande zote mbili kwa makini ili kufikia maamuzi yenye kuleta maridhiano badala ya kuongeza migawanyiko katika familia. Amesema wajumbe wa mabaraza wanapaswa kuzingatia sheria, maadili na utu katika utekelezaji wa majukumu yao.

Katika semina hiyo, washiriki wamepata mafunzo mbalimbali kuhusu mbinu za usikilizaji wa migogoro, namna ya kuendesha vikao vya usuluhishi pamoja na umuhimu wa kutunza siri za wahusika ili kujenga imani kwa wananchi wanaofika kutafuta msaada.

Semina hiyo imeonekana kuwa hatua muhimu katika kuimarisha mfumo wa utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, ambapo viongozi na wataalamu wameendelea kusisitiza umuhimu wa mazungumzo, maridhiano na haki katika kujenga jamii yenye utulivu na mshikamano endelevu ili kufikia Dira ya maendeleo 2050.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button