Kinondoni yazindua hamasa kushangilia Serengeti Boys

DAR ES SAALAAM :MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amewahamasisha wakazi wa Tandale na Kinondoni kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushangilia timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, itakayocheza fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON U-17 dhidi ya Senegal kesho nchini Morocco.

Akizungumza leo Tandale Sokoni, Mtambule amesema Tanzania sasa inajivunia nafasi kubwa kwenye ramani ya michezo duniani, si soka pekee bali hata ngumi, riadha na michezo mingine.

“Tunafahamu Tanzania sasa hivi tunajivunia kwenye ramani ya Afrika, ramani ya dunia, nafasi yetu kimichezo ni kubwa sana. Tumeendelea kukua siku hadi siku. Sio mchezo mmoja tu, ni michezo yote,” alisema.

Alitaja mafanikio ya ngumi kupitia Azam, Mafia Boxing na promoters wengine, huku akipongeza timu za soka za wanaume na wanawake kwa kufanya vizuri.

Ili kuwaunga mkono Serengeti Boys, DC Mtambule alitangaza kuwa Wilaya ya Kinondoni imeandaa eneo maalum la kuangalia mchezo huo moja kwa moja katika Shule ya Msingi Tandale hapo kesho Majira ya jioni

“Tunakata 20 katika wilaya hii ya Kinondoni, tuna mitaa 106. Tukakasema katika maeneo haya yote, hebu twende tukasherehekee tukaangalie mpira huu pale Tandale,” amesema

DC Mtambule amesema shughuli zitaanza mapema kwa burudani ya wanamuziki wa kizazi kipya na muziki wa dansi kabla ya kuanza kwa mchezo.

“Baada ya hapo tunawaambia sasa vijana wetu wanaingia uwanjani, mkiwaacha sasa tuangalie kwenye screen hiyo,” alisema huku akiwahimiza wakazi wa mitaa yote sita ya kata ya Tandale kujitokeza.

Amekumbusha jinsi mashabiki wa Arsenal walivyojikusanya Kijitonyama kushangilia timu yao dhidi ya PSG Ulaya. “Sasa sisi wana Kinondoni tunao vijana wetu, tunao watoto wetu, kesho anaenda kutuwakilisha. Wamefanya kazi kubwa, wamejitoa kwa hali na mali. Kesho ndio siku yao, kesho ndio siku yetu.”

Mkuu huyo wa Wilaya alimpongeza Rais kwa kuwa mwanamichezo namba moja na kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika michezo, akibainisha kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa AFCON mwaka 2027.

“Mwakani 2027 nchi yetu imepata bahati kuwa wenyeji wa mashindano ya AFCON. Na sisi Kinondoni hapa tuna viwanja viwili vinatengenezwa kwa ajili ya mazoezi – Leaders na Viwanja vya Farasi. Vinatengenezwa viwanja vya kisasa kabisa,” amesema

Ameongezea kuwa kuna viwanja vingine kama Uwanja wa Meja Jenerali Mbweni, Uwanja wa KMC na viwanja vya soka la ufukweni maeneo ya Mbweni vinavyoendelea kuimarishwa.

DC Mtambule alihitimisha kwa kutoa pongezi kwa Serengeti Boys kwa kazi nzuri ya kucheza na kuiwakilisha vyema Tanzania.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button