T9 yatangaza fursa za AFCON 2027

WAFANYABIASHARA nchini wametakiwa kuanza Β kujiandaa kunufaika na fursa za kiuchumi zitakazotokana na Michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 itakayofanyika Tanzania, Kenya na Uganda.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Ofisa Mtendaji Mkuu kutoka Kampuni ya habari na mawasiliano T9, Othman Abdulrazak, amesema mashindano hayo yatafungua fursa za uwekezaji, biashara na ajira, hususan kwa vijana.
Amesema T9 imeandaa mfumo wa biashara utakaowaunganisha wafanyabiashara na fursa zitakazojitokeza katika sekta mbalimbali zikiwemo usafirishaji, utalii, malazi, huduma za kifedha, usambazaji wa bidhaa na teknolojia. “AFCON ni fursa kubwa ya kiuchumi. Tukijiandaa mapema na kwa weledi, Tanzania itanufaika na pia itaonyesha uwezo wake wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa,” amesema. SOMA: TTB yatumia sabasaba kukuza utalii, fursa AFCON
Aidha, amesema kampuni hiyo imejenga miundombinu ya kidijitali itakayorahisisha wafanyabiashara kushiriki katika fursa zitakazotokana na matumizi ya wageni watakaohudhuria michuano hiyo.
Pia ametangaza kufanyika kwa Kongamano la Wadau kuelekea AFCON 2027 litakalofanyika Septemba 9 mwaka huu jijini Dar es Salaam, likiwakutanisha wafanyabiashara, wawekezaji na wadau wengine kujadili namna ya kunufaika na fursa za mashindano hayo.



