Ashauri PPP inufaishe pande zote

DAR ES SALAAM: Dk Lutengano Mwinuka ameshauri kuwa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP) unapaswa kunufaisha pande zote mbili zinazoingia makubaliano ya kutekeleza miradi ya kimkakati.
Mhadhiri huyo alitoa maoni hayo wakati akichangia hoja katika mhadhara wa umma uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) ukiangazia nafasi ya PPP katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya mwaka 2050 alisema kuna umuhimu kuhakikisha Serikali na sekta binafsi zote zinanufaika ili ushirikiano huo uwe na tija na uendelevu.
“Bado dhana ya win-win lazima iangaliwe, kwa maana Serikali iweze kufaidika lakini pia sekta binafsi ifaidike ili ubia huo uwe na maana,” amesema.
Ameeleza kuwa dhana ya ubia haipaswi kuangaliwa kwa mtazamo finyu wa makampuni na mashirika pekee, bali inapaswa kutafsiriwa kwa upana zaidi kwa kuhusisha wadau mbalimbali wenye uwezo wa kuchangia maendeleo.
Dk Mwinuka amesema ni wakati wa kupanua wigo wa fikra kuhusu ubia na kutafuta njia mbadala za kushirikiana na wadau tofauti ili kuvutia mitaji na kuwezesha utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.



