ATCL kuanza safari Dar – Urusi Julai 2

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuanza kwa safari za ndege za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow kuanzia Julai 2 mwaka huu, hatua aliyoieleza kuwa itaimarisha biashara, uwekezaji na utalii kati ya Tanzania na Urusi.
Akizungumza katika Jukwaa la Kimataifa la Uchumi la St. Petersburg (SPIEF), Rais Samia alisema Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) litaanza rasmi safari hizo mwezi ujao, huku akieleza kuwa maandalizi pia yanaendelea kwa Shirika la Azur Air kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Moscow kwenda Zanzibar.
“Nina furaha kutangaza kuwa Air Tanzania itaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Moscow. Tarehe 2 Julai itakuwa safari ya kwanza kuelekea Moscow. Pia tunatarajia Azur Air kuanza safari za moja kwa moja kutoka Moscow kwenda Zanzibar,” alisema Rais Samia.
SOMA: ATCL kuongeza safari, kujiendesha kwa tija

Amesema hatua hiyo ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Urusi, hususan katika sekta za biashara na utalii ambazo zimeendelea kukua kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni. Jukwaa hilo la 29 la SPIEF linafanyika kuanzia Juni 3 hadi 6 mwaka huu likiwakutanisha zaidi ya washiriki 20,000 kutoka takribani nchi 76 duniani kujadili masuala mbalimbali ya uchumi wa kimataifa.
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997, SPIEF imeendelea kuwa moja ya majukwaa makubwa ya kimataifa ya majadiliano kuhusu uchumi, biashara na uwekezaji, huku Rais wa Urusi, Vladimir Putin, akishiriki mara kwa mara tangu mwaka 2005.



