Mkuu wa Wilaya Kilombero ahimiza utuzanji mazingira

MOROGORO: MKUU wa Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro, Dunstan Kyobya, amesema mazingira ni msingi wa maendeleo ya taifa na ustawi wa jamii, hivyo ni wajibu wa kila mwananchi kushiriki kuyatunza kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadaye.

Kyobya amesema hayo Juni 5, 2026 aliposhiriki Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambayo hufanyika Juni 5 kila mwaka.

Katika siku hiyo Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) Wilaya ya Kilombero umeadhimisha kwa kupanda miti 1,000 katika maeneo mbalimbali ya wilayani humo.

Mkuu wa Wilaya katika kampeni hiyo, wananchi wakihimizwa kuacha shughuli zinazoharibu mazingira na kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa rasilimali za asili.

Amesema vitendo vya uharibifu wa mazingira vinaendelea kuchangia kupungua kwa vyanzo vya maji, kuongezeka kwa athari za mabadiliko ya tabianchi na kuhatarisha shughuli muhimu za kiuchumi, hususan kilimo na ufugaji.

“Ni wajibu wa kila mmoja wetu kushiriki katika kulinda mazingira kwa kupanda miti, kutunza vyanzo vya maji na kuacha shughuli zinazochangia uharibifu wa mazingira kwani haya ni maeneo muhimu kwa maisha ya sasa na ya baadaye,” amesema Kyobya.

Kyobya aliwataka wananchi kuepuka shughuli za kibinadamu katika maeneo yaliyohifadhiwa na kandokando ya mito, akieleza kuwa maeneo hayo yana mchango mkubwa katika kulinda mifumo ikolojia na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa maji.

Mkuu wa Wilaya aliwahimiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali za kuongeza uoto wa asili kupitia kampeni mbalimbali za upandaji miti zinazolenga kuifanya Tanzania kuwa ya kijani zaidi ifikapo mwaka 2050.

Kwa upande Mhifadhi waTFS Wilaya ya Kilombero,(SCO) Zarina Haridi, amesema zaidi ya miti 1,000 iliyopandwa ni sehemu ya mchango wa wilaya hiyo katika utekelezaji wa kampeni ya kitaifa ya kuimarisha uhifadhi wa mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Amesema Siku ya Mazingira Duniani huadhimishwa kila mwaka kwa lengo la kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda mazingira na kuhamasisha hatua za uhifadhi wa rasilimali za asili kwa maendeleo endelevu.

Maadhimisho ya mwaka huu nchini yamefanyika chini ya kaulimbiu ya “Dira ya 2050: Tunakijanisha Tanzania,” inayolenga kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika urejeshaji wa mifumo ikolojia, utunzaji wa mazingira na kuongeza uoto wa asili nchini.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button