Wanafunzi wa kike wapewa tahadhari matumizi ya simu

MOROGORO: WANAFUNZI wakike wa shule za msingi na sekondari mkoani Morogoro wameshauriwa kujiepusha na matumizi yasiyo sahihi ya simu kwa vile zimebainika ni vichocheo vya wao kujingiza kwenye uhusiano wa kimapenzi wakiwa kwenye umri mdogo, kufanyiwa ukatili wa kigono na wengi wao kupata mimba.
Mwenyekiti wa Kampeni ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA), Mkoa wa Morogoro, Joyce Nyangi ,amesema hayo wakati wa halfa ya ugawaji taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya msingi na sekondari Wilaya ya Kilosa.

Shule nne zikiwemo mbili za msingi na mbili za sekondari, wanafunzi wake wakike zilizipo Kata ya Chanzuru walipatiwa taulo za kike kupitia Taasisi ya Kumbukumbu ya Celina Kombani iliyopo chini ya Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro, Lucy Kombani ambaye ndiye Mkurugenzi Mtendaji wake.
Nyangi amesema kumekuwa na wimbi la wanafunzi wakike kutumia simu janja kuangalia mitandao isiyozingatia maadili na wanajiingiza katika uhusino na wanaume na baadhi yao wakijikuta wakipewa mimba pamoja na kufanyiwa ukatili wa kigono.
“Hatukatai mwanafunzi kuwa simu, jee anaitumiaje, ni kuangalia picha zisizo na maadili zenye vishawishi wao kujaribu mambo yasiyofaa na hili ni moja ya janga kubwa,”amesemaNyangi.
Pia amewahadharisha wasikubali kupewa zawadi na watu wasiowajua msaada wa usafiri kwani ni miongoni mwa si waaminifu wakiwemo baadhi ya madereva wa bodaboda.

Naye, Mhasibu wa Taasisi hiyo, Joyce Mizambwa, katika mada yake kwa wanafunzi kabla ya ugawaji wa taulo za kike amesema hedhi si ugonjwa bali ni utaratibu wa kawaida wa kibiolojia baada ya mwanamke kubalehe , ni usalama na uhai wa afya ya uzazi kwa mtoto wa kike.
“Hedhi salama ni muhimu katika kuboresha afya kwa kuzuia maambukizi, kupunguza harufu mbaya na kufanya wanawake ama wasichana ajisikie vizuri na si ugonjwa,” amesema Mizambwa.
Mizambwa amesema mzunguko wa hedhi huchukua siku 28, na inatofautiana kati ya mtu mmoja na mwingine, na kipindi cha hedhi huwa kwa muda wa siku mbili hadi hadi tano ,na kawaida kwa msichana kwa mara ya kwanza huanza kati ya umri wa miaka 8 na 15.
Kwa upande wake Mwazilishi mwenza wa Taasisi hiyo , Dorisia Edward amewataka wanafunzi wa kike wazingatie usafi wa mwili na mavazi ili kujiepusha na magonjwa hasa wanapokuwa kwenye hedhi.

Dorisia amesema kuwa watoto wengi wakike hawajapata elimu ya namna ya kujisitiri , na kwamba kabla ya ugawaji wa taulo hizo elimu inatolewa kwao ili hedhi isisababishe utoro shuleni .
Nao baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kutoka kata ya Chanzuru kwa nyakati tofauti wamempongeza Mbunge wa Viti Maalum, Lucy Kombani kupitia taasisi yake kuwapatia msaada wa taulo za kike zaidi ya maboksi 53 ili kusaidia kulinda afya zao hasa wanapokuwa shuleni kipindi cha hedhi na kushiriki vyema masomo.



