CCM yawaonya wanaohamasisha uvunjifu wa amani

DODOMA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kitaendelea kuunga mkono juhudi za Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, za kuharakisha maendeleo ya wananchi huku kikisisitiza kuwa amani, umoja na mshikamano ni msingi muhimu wa maendeleo ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma leo Juni 13,2026 Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenani Kihongosi, amesema chama hicho kimeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofanywa na serikali katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji, umeme, barabara, kilimo na uwezeshaji wa wananchi kiuchumi.

Amesema katika ziara za chama zilizofanyika katika mikoa 12 na wilaya 41, viongozi wa CCM wamejionea mafanikio makubwa yaliyopatikana pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi ili kuzitafutia ufumbuzi kupitia serikali.
“Tumeshuhudia kazi kubwa inayofanywa na serikali ya CCM chini ya Rais Samia. Fedha nyingi zimepelekwa katika miradi ya maendeleo na wananchi wanaendelea kunufaika na maboresho ya huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini,” amesema.

Kihongosi amesema pamoja na mafanikio hayo, baadhi ya changamoto zilizobainika ni migogoro ya ardhi, huduma ya maji katika maeneo machache na vitongoji ambavyo bado havijafikiwa kikamilifu na huduma ya umeme, huku akieleza kuwa serikali inaendelea kuzitatua kupitia bajeti na miradi inayoendelea kutekelezwa.
Amesema maendeleo ya taifa hayawezi kupatikana kwa siku moja bali yanahitaji muda, mipango na uwekezaji endelevu, akibainisha kuwa Tanzania ya sasa imepiga hatua kubwa ikilinganishwa na ilivyokuwa miaka mitano au 10 iliyopita.
Aidha, amempongeza Rais Samia kwa kuendelea kufungua fursa za kiuchumi kupitia diplomasia ya kimataifa, hatua ambayo imeongeza uwekezaji na ushirikiano wa maendeleo kwa manufaa ya taifa.
Kuhusu Bajeti ya Serikali ya mwaka 2026/27 ya zaidi ya Sh trilioni 62, Kihongosi alisema bajeti hiyo itaongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuboresha huduma muhimu kwa wananchi, huku akisisitiza kuwa ni ushahidi wa dhamira ya serikali ya kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania.



