Tanzania yaendelea kuwekeza sekta ya bahari

DODOMA; Tanzania inaendelea kuwekeza katika sekta ya bahari, hali inayofungua nafasi zaidi za ajira na ujasiriamali kwa vijana kupitia mafunzo yanayotolewa na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (Dar es Salaam Maritime Institute (DMI)).
Akizungumza katika Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma, Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Mipango, Fedha na Utawala, Profesa Mwisila Lucas, amesema kozi zinazotolewa na chuo hicho zinamwezesha mhitimu kupata ajira rasmi lakini pia kujiajiri, akisisitiza kuwa sekta ya bahari bado ina fursa nyingi ambazo vijana wanapaswa kuzitumia.

Ameongeza kuwa Serikali imeendelea kukiimarisha chuo hicho kwa kukipatia vifaa vya kisasa vya mafunzo ya uhandisi wa bahari, urubani wa meli, usafirishaji na ushughulikiaji wa mizigo bandarini pamoja na maeneo mengine muhimu ya sekta ya majini.
Aidha, amesema chuo kimeongeza wataalamu katika nyanja mbalimbali zikiwemo uhandisi wa bahari, unahodha wa meli, uchumi wa bahari, sheria za bahari na usimamizi wa shughuli za majini ili kuhakikisha kinazalisha wahitimu wenye ujuzi unaohitajika sokoni.

Mbali na mafunzo, chuo kinatoa huduma za ushauri elekezi kwa taasisi za umma na binafsi zinazojihusisha na shughuli za baharini pamoja na kufanya tafiti zinazolenga kuchangia maendeleo ya uchumi wa buluu nchini.
Profesa Lucas amesema ushiriki wa DMI katika maonesho hayo unalenga kusogeza huduma karibu na wananchi na kutoa elimu kuhusu fursa zilizopo katika sekta ya bahari, ambapo wananchi wanapata maelezo ya moja kwa moja kutoka kwa wataalamu.

Amefafanua kuwa dirisha la kwanza la udahili linatarajiwa kufungwa Julai 10 mwaka huu, akiwahimiza wanafunzi waliomaliza kidato cha nne na sita pamoja na wazazi kutembelea tovuti ya chuo hicho kupata taarifa za kozi na vigezo vya kujiunga.
Aidha, amesema wanafunzi watakaodahiliwa wanaweza kunufaika na fursa za mikopo na ufadhili kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB), Mfuko wa Mikopo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mfuko wa Samia Scholarship pamoja na mifuko mingine ya kusaidia wanafunzi wa sekta ya bahari.

Amesema kadri Tanzania inavyoendelea kuwekeza katika uchumi wa buluu, sekta za usafiri wa majini, bandari, uvuvi na biashara zinazohusiana na bahari zinatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayozalisha ajira nyingi zaidi katika miaka ijayo.


